Sefania 2

Sefania 2

Watu wanaonywa, wajute kwa ajili ya mapatilizo yatakayokuja.

1Jikusanyeni, jikusanyeni, mlio taifa lisilokata tamaa,

shauri likiwa halijafanyika bado!

Kwani siku hiyo inakuja mbio kama makapi yapeperushwayo.

2Kwa kuwa makali ya Bwana yenye moto hayajawafikia bado,

kwa kuwa siku ya makali ya Bwana haijawafikia bado,

3mtafuteni Bwana, ninyi wanyenyekevu wote wa nchi hii

mnaoyafanya yanyokayo mbele yake!

Utafuteni wongofu! Utafuteni unyenyekevu nao!

Kwa njia hii labda mtaona pa kujifichia,

siku ya makali ya Bwana itakapotimia.

4Kwani Gaza utakuwa umeachwa, nao Askaloni utakuwa mapori matupu,

Waasdodi watakimbizwa mchana, nao Ekroni utabomolewa.

5Yatawapata nanyi mkaao pwani, mlio wa taifa la Wakreta!

Neno la Bwana litatimia kwenu wa Kanaani,

nako kwenu wa nchi ya Wafilisti kwamba:

Nitakuangamiza, pasisalie mwenyeji.

6Ndipo, nchi ya pwani itakapokuwa nyika

yenye visima na mazizi ya kondoo, watakaowachunga huko.

7Nchi hii itakuwa yao wakaosalia wa mlango wa Yuda;

wao ndio watakaochunga huko,

tena jioni watakwenda kulala katika nyumba za Askaloni;

kwani Bwana Mungu wao atawakagua,

ayafungue tena mafungo yao.

8Nimeyasikia matusi ya Wamoabu

nao ufyozaji wa wana wa Amoni,

wakiwatukana walio ukoo wangu

na kujivuna kwa kuingia katika mipaka yao.

9Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli:

Kweli kwa hivyo, nilivyo Mwenye uzima,

nchi ya Moabu itakuwa kama Sodomu

nayo nchi ya wana wa Amoni kama Gomora,

zitageuka kuwa kwenye viwawi,

zitakuwa mashimo ya chumvi na mapori matupu kale na kale.

Masao yao walio ukoo wangu watawanyang'anya mali zao,

watakaosalia wa taifa langu watawachukua, wawe watumwa wao.

10Hayo yatawapata kwa ajili ya majivuno yao, kwani wamejikuza na kuwatukana walio ukoo wa Bwana Mwenye vikosi na kuwazomea.

11Bwana ataogopwa kwao, kwani miungu yote ya hapa nchini ataitowesha, wamwangukie wote, kila mtu mahali pake, hata visiwa vyote vya wamizimu.

12Nanyi Wanubi, mtapigwa na upanga wangu, mfe.[#Ez. 30:9.]

13Kisha ataukunjua mkono wake na kuuelekeza kaskazini, awaangamize Waasuri, nao Niniwe ataugeuza kuwa mapori matupu na nchi kavu kama nyika.[#Nah. 1:1.]

14Mwake yatalala makundi mazima ya kila nyama wa nchi za mataifa, hata korwa na nungu watalala katika vichwa vya nguzo zake, sauti za bundi zitasikilika madirishani, penye vizingiti patajaa takataka, kwani mbao za miangati zitakuwa zimeondolewa.[#Yes. 13:21; 34:11.]

15Hayo ndiyo yatakayoupata huo mji uliojaa furaha uliokaa pasipo kuhangaika kabisa, uliosema moyoni mwake: Mji ni mimi, hakuna mwingine tena! Kumbe umegeuka kuwa mapori matupu na makao ya nyama wa porini! Kila atakayepapita atauzomea na kuupungia kwa mkono wake.[#Yes. 47:8.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania