The chat will start when you send the first message.
1Baada ya siku si nyingi mfalme alituma mzee mmoja Mwathene kuwashurutisha Wayahudi kuziacha amri za baba zao, wasizifuate amri za Mungu.
2Tena, alitie unajisi hekalu la Yerusalemu na kuliita kwa jina la Zeu wa Olimpo; na lile la Gerizimu liitwe kwa jina la Zeu Mlinzi wa Wageni, kama walivyotaka wale waliokaa huko.
3Matokeo ya jambo hilo yalikuwa maovu na kuchukiza kabisa.
4Maana hekalu lilijaa ghasia na ufisadi wa watu wa mataifa waliobembelezana na makahaba na kutembea na wanawake katika nyua zake takatifu. Tena, waliingiza vitu vilivyo haramu,
5hata madhabahu ilijaa dhabihu za kuchukiza zilizokatazwa na sheria.
6Haikuwezekana kuishika Sabato, wala kuziadhimisha sikukuu za zamani, wala hata kujitaja kwa wazi kuwa Myahudi.
7Kila mwezi, katika sikukuu ya Dioniso walishurutishwa kuandamana kwa heshima ya Dioniso wakivaa taji za majani.
8Pia, kwa shauri la Tolemayo, maagizo yalipelekwa kwenye miji ya Kigiriki ya karibu wawafanyie Wayahudi vivyo hivyo na kuwashurutisha kula dhabihu.
9Na wale wasiokubali kuzifuata kawaida za Kigiriki wauawe. Hali yao mbaya ilikuwa dhahiri kwa wote.
10Maana wanawake wawili walihukumiwa kwa kuwatahiri watoto wao, nao walipokwisha kutembezwa mjini, watoto wakining'inia maziwani mwao, walitupwa chini kutoka juu ya ukuta.[#1 Mak 1:60-61]
11Wengine waliokimbilia mapango ya karibu ili kuishika siku ya saba kwa siri walisalitiwa kwa Filipo na kuchomwa moto wote pamoja, kwa sababu waliona si halali kujipigania katika siku hiyo takatifu.[#1 Mak 2:32-33]
12Lakini nawasihi wasomaji wa kitabu hiki, wasikate tamaa kwa sababu ya misiba hiyo, bali wafahamu kwamba kusudi la adhabu hizi halikuwa kuwaharibu watu wetu, ila kuwaadilisha.
13Maana, kwa kweli, ni dalili ya upendo wakosaji wasiachwe kwa muda mrefu bila kuonywa upesi.
14Kwa habari za mataifa mengine, BWANA Mwenyezi huwaonesha uvumilivu mwingi, asiwaadhibu mpaka wamefikia kikomo cha uovu wao.
15Lakini kwetu nia yake ni mbali, yaani asilazimike kutupatiliza baadaye dhambi zetu zitakapokomaa.
16Kwa hiyo hatuondolei rehema zake wakati wowote; ingawa anawapiga watu wake kwa mateso, lakini hawaachi kabisa.
17Haya twayasema kwa kuwakumbusheni tu; basi, baada ya maneno hayo machache, tuendelee na masimulizi yetu.
18Eleazari, mmoja wa waandishi wakuu, mtu wa umri mkubwa na sura njema, alishurutishwa kufunua kinywa chake kulishwa nyama ya nguruwe.[#Law 11:7-8; Ebr 11:35]
19Lakini akaitema ile nyama, akasogea mwenyewe kwenye mahali pa kuteswa, akiona afadhali kufa kwa heshima kuliko kuishi kwa unajisi.
20Akatenda kama yampasavyo mtu aliyekaza nia yake kuvikataa vitu zisivyo halali kuonjwa hata kwa kutaka kujiokoa maisha.
21Basi, wale waliosimamia dhabihu hiyo haramu, kwa kuwa wamejuana naye kwa miaka mingi, walimchukua kando wakamsihi alete nyama yake mwenyewe, iliyo halali ya kuliwa, na kufanya kana kwamba anaila nyama ya dhabihu, kama mfalme alivyoamuru.
22Hivyo atajiponya na mauti, na kutendewa nao kwa hisani kwa sababu ya urafiki wao wa tangu zamani.
23Lakini yeye aliikaza nia yake madhubuti, nia iliyostahili umri wake na jadi yake, na mvi zake stahivu, na mwendo wake wa adili tangu utoto wake katika kuzishika amri takatifu zilizotolewa na Mungu. Akakataa kabisa, na kuwaambia wampeleke kuzimuni upesi, akisema:
24Haipatani na miaka yetu kudanganya, isije vijana wengi wakadhani ya kuwa Eleazari, katika mwaka wake wa tisini, ameiacha dini yake kwa dini ya kigeni;
25na hivyo, kwa sababu ya udanganyifu wangu, watapotoshwa, na mimi mwenyewe nitajipatia unajisi na aibu katika uzee wangu.
26Na hata nikiepukana na adhabu ya wanadamu sasa, lakini sitaweza kuepukana na mikono ya Mwenyezi, nikiwa hai au nimekufa.
27Basi, nikitoa maisha yangu sasa kwa ushujaa, nitajionesha kuwa nimeistahili miaka yangu mingi,
28na kuwaachia vijana mfano wa kufa mauti ya fahari kwa hiari na kwa uthabiti, kwa ajili ya amri takatifu zenye heshima. Alipokwisha kusema hayo, alipaendea mara mahali pa kuteswa.
29Nao waliokuwa wakimwonesha urafiki walibadili nia zao kwa mabaya kwa sababu ya maneno yake waliyoyaona kuwa ya kiwazimu.
30Naye alipokuwa kufani kwa ajili ya mapigo yake, aliugua akasema, Kwake Bwana ajuaye yote ni dhahiri ya kuwa ingawa ningaliweza kuepukana na mauti, lakini ninavumilia maumivu makali mwilini mwangu; hata rohoni mwangu ninayavumilia kwa furaha kwa sababu ya kicho changu kwake.
31Hivyo alikufa; na kwa kufa kwake aliacha mfano wa unyofu na ukumbusho wa wema, si kwa vijana tu, ila kwa jamii yote ya taifa lake.