The chat will start when you send the first message.
1Basi Daudi akamwambia BWANA maneno ya wimbo huu, siku ile BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na mkononi mwa Sauli;[#Kut 15:1]
2akasema,[#Mwa 15:1; Kum 32:4; 1 Sam 2:2; Zab 18:2; 91:2; Mit 18:10; Mt 18:11]
BWANA ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu,
3Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye;[#Ebr 2:13; Mwa 15:1; Zab 3:3; Mit 30:5; Lk 1:69; Mit 18:10; Zab 9:9; 18:2; Isa 32:2; Isa 32:2; Yer 16:19]
Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na
kimbilio langu;
Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri.
4Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa;
Hivyo nitaokoka na adui zangu.
5Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka,
Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
6Kamba za kuzimu zilinizunguka;
Mitego ya mauti ikanikabili.
7Katika shida yangu nilimwita BWANA,[#Zab 116:4; Yon 2:2; Kut 3:7]
Naam, nikamlalamikia Mungu wangu;
Naye akaisikia sauti yangu hekaluni mwake,
Kilio changu kikaingia masikioni mwake.
8Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka,[#Amu 5:4; Ayu 26:11; Zab 18:7; 77:18]
Misingi ya mbinguni ikasukasuka
Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu.
9Kukapanda moshi kutoka puani mwake,[#Zab 97:3; Hab 3:5; Ebr 12:29]
Moto ukatoka kinywani mwake ukala;
Makaa yakawashwa nao.
10Aliziinamisha mbingu akashuka;[#Isa 64:1]
Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake.
11Akapanda juu ya kerubi akaruka;[#Zab 104:3]
Naam, alionekana juu ya mabawa ya upepo.
12Akafanya giza hema zake za kumzunguka,
Makusanyiko ya maji, mawingu makuu ya mbinguni.
13Toka mwangaza uliokuwa mbele zake
Makaa ya moto yakawashwa.
14BWANA alipiga radi toka mbinguni,[#Isa 30:30]
Naye Aliye Juu akaitoa sauti yake.
15Akapiga mishale, akawatawanya;[#Kum 32:23; Zab 7:13; 77:17; Hab 3:11]
Umeme, naye akawatimua.
16Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari,
Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa,
Kwa kukemea kwake BWANA,
Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake.
17Alipeleka kutoka juu, akanishika;
Akanitoa katika maji mengi;
18Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu,
Na wale walionichukia;
Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.
19Walinikabili siku ya msiba wangu;
Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu.
20Akanitoa akanipeleka panapo nafasi;[#Zab 31:8; 2 Sam 15:26]
Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.
21BWANA alinitendea kulingana na haki yangu;
Kulingana na usafi wa mikono yangu akanilipa.
22Maana nimezishika njia za BWANA,
Wala sikumwasi Mungu wangu.
23Maana hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu;[#Kum 7:12]
Na kuhusu amri zake, sikuziacha.
24Nami nilikuwa mkamilifu kwake,[#Mwa 6:9; Ayu 1:1; Yn 1:47]
Nikajilinda na uovu wangu.
25Basi BWANA amenilipa kulingana na haki yangu;
Kulingana na usafi wa mikono yangu mbele zake.
26Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili[#Mt 5:7]
Kwa mkamilifu utajionesha kuwa mkamilifu;
27Kwake ajitakasaye utajionesha kuwa mtakatifu;[#Law 26:23]
Na kwa mpotovu utajionesha kuwa mkaidi.
28Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa;[#Kut 3:7; Zab 12:5; Mt 5:3]
Ila macho yako huwapinga wenye kiburi, uwadhili.
29Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee BWANA;
Na BWANA ataniangazia giza langu.
30Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi;
Kwa msaada wa Mungu wangu ninaruka ukuta.
31Mungu njia yake ni kamilifu;[#Kum 32:4; Dan 4:37; Ufu 15:3; Zab 12:6; Mit 30:5]
Ahadi ya BWANA imehakikishwa;
Yeye ndiye ngao yao
Wote wanaomkimbilia.
32Maana ni nani aliye Mungu, ila BWANA?[#Kum 32:31; 1 Sam 2:2; Isa 45:5,6]
Ni nani aliye mwamba, ila Mungu wetu?
33Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu;[#Zab 27:1; Kum 18:13]
Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake.
34Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu;[#Hab 3:19]
Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.
35Ananifundisha mikono yangu vita;
Hata mikono yangu inaupanda upinde wa shaba.
36Nawe umenipa ngao ya wokovu wako;
Na unyenyekevu wako umenikuza.
37Umezifanyia nafasi hatua zangu,
Wala miguu yangu haikuteleza.
38Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza;
Wala sikurudi nyuma hadi walipokomeshwa.
39Nami nimewakomesha na kuwapiga wasiweze kusimama;
Naam, wameanguka chini ya miguu yangu.
40Maana umenijaza nguvu ya kupigana vita;
Ukawafanya adui zangu wafifie chini yangu.
41Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo,
Ili niwakatilie mbali wanaonichukia.
42Walitazama, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa;[#1 Sam 28:6; Ayu 27:9; Mit 1:28]
Walimwita BWANA, lakini hakuwajibu.
43Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi,
Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya.
44Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu;[#Kum 28:13; Isa 55:5]
Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa;
Watu nisiowajua watanitumikia.
45Wageni walinijia wakinyenyekea;
Mara tu waliposikia habari zangu,
Walinitii.
46Wageni nao waliishiwa nguvu,[#Mik 7:17]
Wakatoka katika ngome zao wakitetemeka.
47BWANA yu hai;[#Zab 89:26]
Na ahimidiwe mwamba wangu;
Na atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu;
48Naam, Mungu anilipiziaye kisasi,[#Zab 144:2]
Na kuwatweza watu chini yangu,
49Na kuniokoa kutoka kwa adui zangu;
Naam, waniinua juu yao walioniinukia;
Ukaniokoa kutoka kwa watu wajeuri.
50Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa,[#Rum 15:9]
Nami nitaliimbia jina lako.
51Yeye ni mnara wa wokovu kwa mfalme wake;[#22:51 Au wokovu mkuu.]
Amfanyia fadhili masihi wake,
Kwa Daudi na wazawa wake, hata milele.