2 Samweli 23

2 Samweli 23

Maneno ya mwisho ya Daudi

1Basi haya ndiyo maneno ya mwisho ya Daudi.

Daudi, mwana wa Yese, anena,

Anena huyo mtu aliyeinuliwa juu,

Yeye, masihi wake Mungu wa Yakobo,

Mtungaji wa nyimbo za Israeli mwenye kupendeza;

2Roho ya BWANA ilinena ndani yangu,[#2 Pet 1:21]

Na neno lake likawa ulimini mwangu.

3Mungu wa Israeli alisema,[#Kut 18:21]

Mwamba wa Israeli aliniambia,

Atawalaye wanadamu kwa haki,

Akitawala katika kicho cha Mungu,

4Atakuwa kama nuru ya asubuhi jua lichapo,[#Mit 4:18]

Asubuhi isiyo na mawingu.

Likichipuza mimea ardhini,

Kwa mwangaza baada ya mvua;

5Je! Sivyo ilivyo nyumba yangu mbele za BWANA?[#1 Fal 9:4-6]

Kwa kuwa amefanya nami agano la milele;

Ina taratibu katika yote, ni thabiti,

Maana ni wokovu wangu wote, na shauku langu lote.

6Lakini hatawachipuza watu wasiofaa;

Watakuwa wote kama miiba ya nyikani ya kutupwa,

Maana haichukuliki kwa mkono,

7Mtu atakayeigusa hiyo,

Na awe na chuma na mpini wa mkuki,

Nao watateketezwa papo hapo kwa moto.

Mashujaa wa Daudi

8Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni, Hamkuu wa wakuu wa majeshi; huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja.[#23:8 Au, Yosheb-bashebethi.]

9Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;[#1 Nya 11:12; 27:4]

10huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye BWANA akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu.

11Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo shamba lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti;[#1 Nya 11:12]

12ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye BWANA akafanya wokovu mkuu.

13Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka, wakamwendea Daudi wakati wa mavuno mpaka pango la Adulamu, na kikosi cha Wafilisti walikuwa wamefanya kambi katika bonde la Warefai.[#1 Nya 11:15; 14:9; Kum 33:29; 1 Sam 22:1; 1 Nya 29:11; 2 Nya 14:11-14; 25:8; Zab 3:8; 46:1; Mit 21:30,31; Rum 8:31; 2 Sam 5:18; Isa 17:5]

14Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati ule walikuwako Bethlehemu.[#1 Sam 22:4; 1 Nya 12:16]

15Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango!

16Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilichokuwa karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; lakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za BWANA.

17Akasema, Hasha, BWANA, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatarisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu.[#Law 17:10]

18Tena, Abishai, nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa wale watatu. Huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua, akawa na jina kati ya wale watatu.[#2 Sam 2:18; 1 Nya 11:20]

19Je! Huyo hakuwa na heshima maalumu miongoni mwa wale watatu? Kwa hiyo akawekwa kuwa kamanda wao; ila hakuweza kuwa kama wale watatu.

20Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wawili wakali wa Moabu, pia aliingia katika shimo na kumwua simba wakati wa theluji;[#Yos 15:21; Kut 15:15; #23:20 Au, wana wawili wa Arieli, wa Moabu.]

21huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyang'anya Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe.[#1 Nya 11:23]

22Hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu.

23Alikuwa mwenye heshima kuliko wale thelathini, ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Naye Daudi akamteua kuwa mkuu wa walinzi wake.[#2 Sam 8:18]

24Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa mmojawapo wa wale thelathini; na Elhanani, mwana wa Dodo, wa Bethlehemu;[#2 Sam 2:18]

25na Shama, Mharodi, na Elika, Mharodi;[#1 Nya 11:27]

26na Helesi, Mpeloni, na Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoi;

27na Abiezeri, Mwanathothi, na Sibekai, Mhushathi;

28na Salmoni, Mwahohi, na Maharai, Mnetofathi;

29na Heledi, mwana wa Baana, Mnetofathi, na Itai, mwana wa Ribai, wa Gibea wa wana wa Benyamini;

30na Benaya, Mpirathoni, na Hurai, wa vijito vya Gaashi;[#Amu 12:15; 2:9]

31na Abieli, Mwarbathi, na Azmawethi, Mbarhumi;

32na Eliaba, Mshaalboni, na wana wa Yasheni; na Yonathani,

33mwana wa Shama, Mharari, na Ahiamu, mwana wa Shalali, Mharari;

34na Elifeleti, mwana wa Ahasbai, na Heferi, Mmaakathi, na Eliamu, mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;

35na Hezro, Mkarmeli, na Paarai, Mwarbi;

36na Igali, mwana wa Nathani, wa Soba, na Bani, Mgadi;

37na Seleki, Mwamoni, na Naharai, Mbeerothi, ambao ni wachukua silaha wa Yoabu, mwana wa Seruya;

38na Ira, Mwithri, na Garebu, Mwithri;[#2 Sam 20:26; Yos 15:48]

39na Uria, Mhiti; idadi yao ilikuwa watu thelathini na saba.[#2 Sam 11:3,6]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya