2 Samweli 7

2 Samweli 7

Agano la Mungu na Daudi

1Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote,[#1 Nya 17:1; Dan 4:29,30]

2mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.[#2 Sam 5:11; Kut 26:1; 40:21]

3Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yuko pamoja nawe.[#1 Fal 8:17; 1 Nya 22:7; 28:2]

4Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema,

5Nenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake?

6Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.[#1 Fal 8:16]

7Mahali kote nilikokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lolote na mtu yeyote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi?[#Law 26:11; Kum 23:14; 2 Sam 5:2; Zab 78:72; Eze 34:2,15,23; Mt 2:6; Mdo 20:28; 1 Pet 5:2]

8Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nilikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;

9nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani.[#Mwa 12:2; 1 Nya 17:8; Lk 1:52]

10Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza;[#Zab 44:2; 80:8; Yer 24:6; Amo 9:15]

11naam, kama ilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote.

Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba.

12Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake.[#Zab 89:3-4; 132:11; Yn 7:42; Mdo 2:30; 13:36; 1 Fal 2:1; 8:20; Kum 31:16; Isa 11:1-3,10]

13Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele.[#1 Fal 5:5; Zab 89:4]

14Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu;[#Zab 89:26-27,30; 2 Kor 6:18; Ebr 1:5]

15lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako.[#1 Sam 15:23]

16Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitaimarishwa milele.[#Zab 89:36-37; Yn 12:34]

17Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.

Ombi la Daudi

18Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa?[#Mwa 32:10]

19Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana MUNGU; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumishi wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana MUNGU.[#Isa 55:8]

20Na mimi, Daudi, nikuambie nini tena zaidi? Iwapo wewe umemjua mtumishi wako, Ee Bwana MUNGU.[#Mwa 18:19; Zab 139:1]

21Kwa ajili ya neno lako, na kwa moyo wako mwenyewe, umetenda makuu hayo yote, ili umjulishe mtumishi wako.[#Efe 4:32]

22Kwa hiyo, wewe ndiwe mkuu, Ee BWANA Mungu, kwa maana hakuna kama wewe, wala hapana Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu.[#1 Nya 16:25; 2 Nya 2:5; Zab 48:1; 86:10; Yer 10:6; Kum 3:24; 4:35; 1 Sam 2:2; Zab 86:8; 89:6; Isa 45:5]

23Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako, mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri wawe wako, kutoka katika mataifa na miungu yao.[#Kum 4:7,34; 33:29; Zab 147:20; Neh 1:10]

24Nawe ulijifanyia imara watu wako wa Israeli, wawe watu wako milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao.[#Kum 26:18]

25Basi sasa, Ee BWANA Mungu, neno lile ulilolinena kuhusu mtumishi wako, na kuhusu nyumba yangu, uliimarishe milele, ukatende kama ulivyosema.

26Jina lako na litukuzwe milele, kwa kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumishi wako, Daudi, itaimarika mbele zako.[#Zab 72:19; Mt 6:9]

27Kwa kuwa wewe, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumishi wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumishi wako, nimepata ujasiri nikuombe ombi hili.

28Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumishi wako jambo hili jema[#Yn 17:17]

29basi, sasa, uwe radhi, ukaibariki nyumba ya mtumishi wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumishi wako na ibarikiwe milele.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya