Ezekieli 32

Ezekieli 32

Maombolezo juu ya Farao na Misri

1Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,

2Mwanadamu, mfanyie Farao, mfalme wa Misri, maombolezo, umwambie, Ulifananishwa na mwanasimba wa mataifa; lakini umekuwa kama joka katika bahari; nawe watoka kwa nguvu pamoja na mito yako, na kuyachafua maji kwa miguu yako, na kuitia uchafu mito yao.[#Eze 27:2; 19:3,6; 29:3; 34:18]

3Bwana MUNGU asema hivi; Nitautanda wavu wangu juu yako, kwa kusanyiko la watu wa kabila nyingi; nao watakuvua katika jarife langu.[#Eze 12:13]

4Nami nitakuacha juu ya nchi kavu, nitakutupa juu ya uso wa uwanda, nami nitawaleta ndege wote wa angani watue juu yako, nami nitawashibisha wanyama wa dunia yote kwako wewe.[#1 Sam 17:44-46; Isa 14:19; Yer 8:2; Eze 29:5; 39:4]

5Nami nitaweka nyama yako juu ya milima, na kuyajaza mabonde kwa urefu wako.[#Eze 31:12]

6Tena kwa damu yako nitainywesha nchi, ambayo waogelea juu yake, hata milimani; na mifereji ya maji itajawa nawe.

7Nami nitakapokuzimisha, nitazifunika mbingu, na kuzifanya nyota zake kuwa giza; nami nitalifunika jua kwa wingu, wala mwezi hautatoa nuru yake.[#Yoe 2:31; Amo 8:9; Isa 13:10; Mt 24:29; Mk 13:24-25; Lk 21:25; Ufu 6:12-13; 8:12]

8Mianga yote ya mbinguni iangazayo nitaifanya kuwa giza juu yako, nami nitatia giza katika nchi yako, asema Bwana MUNGU.

9Tena nitawakasirisha watu wengi mioyo yao, nitakapoleta uangamivu wako kati ya mataifa, uingie katika nchi ambazo hukuzijua.

10Nami nitawashangaza watu wa kabila nyingi kwa habari zako, na wafalme wao wataogopa sana kwa ajili yako, nitakapoutikisa upanga wangu mbele yao; nao watatetemeka kila dakika, kila mtu kwa ajili ya uhai wake, katika siku ya kuanguka kwako.[#Eze 27:35; 26:16]

11Maana Bwana MUNGU asema hivi; Upanga wa mfalme wa Babeli utakujia.[#Yer 46:26]

12Kwa panga za mashujaa nitawaangusha watu wako umati wote; hao wote ni watu wa mataifa watishao, nao watakiharibu kiburi cha Misri, na jamii ya watu wake wengi wataangamia.[#Eze 28:7; 29:19]

13Tena nitawaangaza mifugo wake wote, toka kando ya maji mengi; na mguu wa mwanadamu hautayatibua tena, wala kwato za mnyama hazitayatibua.[#Eze 29:11]

14Ndipo nitakapoyafanya maji yao kuwa safi, na kuiendesha mito yao kama mafuta, asema Bwana MUNGU.

15Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa na jangwa, nchi iliyopungukiwa na vitu vilivyoijaza, nitakapowapiga watu wote wakaao ndani yake, ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA.[#Kut 7:5; Zab 9:16; Eze 6:6,7]

16Hayo ndiyo maombolezo watakayoimba; binti za mataifa watayaimba; kwa hayo wataomboleza kwa ajili ya Misri, na kwa ajili ya watu wake umati wote, asema Bwana MUNGU.[#2 Sam 1:17; 2 Nya 35:25; Eze 26:17]

Maombolezo juu ya Misri

17Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la BWANA likanijia kusema,

18Mwanadamu, walilie watu wa Misri. Wote jamii ukawabwage, naam, yeye, na binti za mataifa mashuhuri, hata pande za chini za nchi, pamoja na watu washukao shimoni.[#Yer 1:10; Eze 26:20]

19Umemshinda nani kwa uzuri? Shuka, ukalazwe pamoja na wasiotahiriwa.[#Eze 31:2; 28:10]

20Wataanguka kati ya watu waliouawa kwa upanga; ametolewa apigwe na upanga; mvuteni aende mbali pamoja na watu wake wote jamii.

21Walio hodari watasema naye, toka kati ya kuzimu pamoja nao wamsaidiao; wameshuka wamelala kimya, hata wasiotahiriwa, wakiwa wameuawa kwa upanga.[#Isa 1:31; 2 Fal 25:3-10; Yer 39:2-8; 52:4-14]

22Ashuru yuko huko, na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga,

23ambao makaburi yao yamewekwa pande za shimo zilizo mbali sana, umati wote wamezunguka kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, waliotisha katika nchi yao walio hai.[#Isa 14:15]

24Elamu yuko huko, na watu wake umati wote, pande zote za kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, walioshuka wakiwa hawajatahiriwa hadi pande za chini ya nchi; ambao waliwatia watu hofu katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni.[#Yer 49:34]

25Wamemwekea kitanda kati ya hao waliouawa, pamoja na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana vitisho vyao vilifanyika katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni; amewekwa kati ya hao waliouawa.

26Mesheki yuko huko, na Tubali, na watu wake umati wote; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana walitisha katika nchi ya walio hai.[#Mwa 10:2; Eze 27:13]

27Je! Wasilale pamoja na mashujaa wao wasiotahiriwa, walioanguka, walioshuka kuzimu pamoja na silaha zao za vita, ambao wameweka panga zao chini ya vichwa vyao, na maovu yao mifupani mwao? Maana waliwatisha mashujaa katika nchi ya walio hai.[#Isa 14:18]

28Lakini utavunjika kati ya hao wasiotahiriwa, nawe utalala pamoja nao waliouawa kwa upanga.

29Edomu yuko huko, wafalme wake, na wakuu wake wote, ambao katika uwezo wao wamelazwa pamoja nao waliouawa kwa upanga; watalala pamoja na hao wasiotahiriwa, na pamoja na hao washukao shimoni.[#Eze 25:12]

30Wakuu wa kaskazini wako huko, wote pia, na Wasidoni, wote walioshuka pamoja na hao waliouawa; kwa sababu ya hofu waliyoleta katika uwezo wao wamefedheheka, nao wamelala wakiwa hawajatahiriwa, pamoja nao waliouawa kwa upanga, nao wanachukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni.[#Eze 38:6,15; 28:21]

31Farao atawaona, naye atapata faraja juu ya watu wake umati wote; naam, Farao, jeshi lake lote waliouawa kwa upanga, asema Bwana MUNGU.[#Eze 14:22]

32Kwa maana nimeweka utisho wake katika nchi ya walio hai; naye atalazwa kati yao wasiotahiriwa, pamoja na hao waliouawa kwa upanga; yeye Farao na watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya