The chat will start when you send the first message.
1Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na silaha ya kuangamiza mkononi mwake.[#Zab 103:20]
2Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja akiwa na silaha yake ya kuua mkononi; na mtu mmoja kati yao akiwa amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba.[#Law 16:4]
3Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni.
4BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaopiga kite na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake.[#Zab 119:53; Ufu 7:3; 9:4; 14:1]
5Na hao wengine aliwaambia, nami nilisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma;
6Waueni kabisa, wazee, na viijana, na wasichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu yeyote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba.[#Ufu 9:4; Yer 25:29; Lk 12:47]
7Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, nendeni. Wakaenenda, wakaua watu katika mji.
8Tena ikawa, walipokuwa wakiwaua, nami nikaachwa, nilianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?[#Hes 14:5; Kum 9:18; Yos 7:6]
9Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, BWANA ameiacha nchi hii, naye BWANA haoni.[#2 Fal 21:16; Zab 10:11; Isa 29:15]
10Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitakuwa na huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao.[#Kum 32:41]
11Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.