Wagalatia 5

Wagalatia 5

1Katika uhuru huo Kristo alituweka huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.[#Gal 4:5,31; Mdo 15:10]

Asili ya uhuru wa Mkristo

2Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidi neno.[#2 Kor 10:1]

3Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote.

4Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema.

5Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani.

6Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutotahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.[#Gal 6:15; 1 Kor 7:19]

7Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli?

8Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi.[#Gal 1:6]

9Chachu kidogo huchachua donge zima.[#1 Kor 5:6]

10Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewasumbua atachukua hukumu yake, awaye yote.[#Gal 1:7; 2 Kor 11:15]

11Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Kwa kufanya hivyo kikwazo cha msalaba kimeondolewa![#1 Kor 1:23]

12Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao![#Zab 12:3]

13Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.[#1 Pet 2:16]

14Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.[#Law 19:18]

15Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana.

Kazi za kimwili

16Basi nasema, Nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.

17Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.[#Rum 7:15-23; Yak 4:5; 1 Pet 2:11]

18Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.[#Rum 8:14]

19Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,[#1 Kor 6:9,10]

20ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, mafarakano, uzushi,

21husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.[#Efe 5:5; Ufu 22:15]

Tunda la Roho

22Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,[#Efe 5:9]

23upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.[#1 Tim 1:9]

24Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.[#Rum 6:6; Kol 3:5; 1 Pet 2:11]

25Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.[#Rum 8:4]

26Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.[#Flp 2:3]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya