Hosea 13

Hosea 13

Hukumu kali kwa Israeli

1Efraimu aliponena, palikuwa na tetemeko; alijitukuza katika Israeli; Lakini alipokosa katika Baali, alikufa.[#Mit 18:12; 2 Fal 17:16]

2Na sasa wanazidi kufanya dhambi, nao wamejifanyia sanamu kwa fedha yao, naam, sanamu kwa kadiri ya akili zao; zote pia ni kazi ya mafundi; nao huzitaja hivi, Wanaume watoao dhabihu na wazibusu ndama.

3Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi, na kama umande utowekao upesi, kama makapi yaliyopeperushwa na tufani sakafuni, na kama moshi utokao katika bomba.

4Lakini mimi ni BWANA, Mungu wako tangu nchi ya Misri; wala hutamjua mungu mwingine ila mimi; wala zaidi ya mimi hakuna mwokozi.

5Mimi nilikujua katika jangwa, katika nchi yenye ukame.[#Kum 8:11-17]

6Kwa kadiri ya malisho yao, kwa kadiri iyo hiyo walishiba; walishiba na moyo wao ukatukuka; ndiyo sababu wamenisahau mimi.

7Basi nimekuwa kama simba kwao; kama chui nitavizia njiani;

8nitawajia kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake; nami nitararua nyama ya mioyo yao; na huko nitawala kama simba; huyo mnyama mkali atawararua.

9Haya ndiyo maangamizo yako, Ee Israeli, kwa kuwa wewe u kinyume changu mimi, kinyume cha msaada wako.

10Yuko wapi sasa mfalme wako, apate kukuokoa katika miji yako yote? Na hao waamuzi wako, uliowanena hivi, Nipe mfalme na wakuu?[#1 Sam 8:5-6]

11Nimekupa mfalme katika hasira yangu, nikamwondoa katika ghadhabu yangu.[#1 Sam 10:17-24; 8:7; 15:26]

12Uovu wa Efraimu umefungwa kwa kukazwa; dhambi yake imewekwa akiba.[#Kum 32:34]

13Uchungu wa mwanamke mwenye mimba utampata; yeye ni mwana asiye na akili; maana wakati umewadia, ambao haimpasi kukawia mahali wapenyapo watoto.

14Nitawakomboa kwa nguvu za kaburi; nitawaokoa kutoka kwa mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Huruma itafichika machoni mwangu.[#Isa 25:8; 26:19; 1 The 4:14-17; Ufu 21:4; Rum 11:29; 1 Kor 15:55]

15Ajapokuwa yeye ni mwenye kuzaa sana kati ya ndugu zake, upepo wa mashariki utakuja, hiyo pumzi ya BWANA itokayo upande wa nyikani, na kijito chake cha maji kitakauka, na chemchemi yake itakaushwa; yeye atateka nyara hazina ya vyombo vyote vipendezavyo.

16Samaria atachukua hatia yake; kwa maana amemwasi Mungu wake; wataanguka kwa upanga; watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande, na wanawake wao wenye mimba watatumbuliwa.[#2 Fal 18:12]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya