Isaya 39

Isaya 39

Wajumbe kutoka Babeli wakaribishwa

1Wakati huo Merodak-baladani, mwana wa Baladani, mfalme wa Babeli, alipeleka barua na zawadi kwa Hezekia; kwa maana amepata habari kwamba amekuwa mgonjwa, na kwamba amepona.[#2 Fal 20:12]

2Hezekia akawafurahia, akawaonesha nyumba yake yenye vitu vyake vya thamani, fedha na dhahabu, na manukato, na marhamu ya thamani, na nyumba yote yenye silaha zake za vita, na vitu vyote vilivyoonekana katika hazina zake; hapakuwa na kitu nyumbani mwake wala katika ufalme wake ambacho hakuwaonesha.[#2 Nya 32:31]

3Ndipo Isaya nabii akamwendea mfalme Hezekia, akamwambia, Watu hawa walisema nini? Nao wametoka wapi kuja kwako? Hezekia akasema, Wametoka katika nchi iliyo mbali, wakaja kwangu toka Babeli.

4Ndipo akasema, Wameona nini katika nyumba yako? Hezekia akajibu, Wameviona vitu vyote vilivyomo nyumbani mwangu; hapana kitu katika hazina zangu ambacho sikuwaonesha.

5Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, Basi, lisikie neno la BWANA wa majeshi.

6Tazama, siku zinakuja, ambazo vitu vyote vilivyomo nyumbani mwako, na hivyo vilivyowekwa akiba na baba zako hata leo, vitachukuliwa mpaka Babeli; hapana kitu chochote kitakachosalia; asema BWANA.[#Law 26:33; Kum 28:64; 1 Fal 14:15; 2 Nya 36:18; Amo 5:27]

7Na baadhi ya wana wako utakaowazaa, watakaotoka kwako, watawachukulia mbali; nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.[#Dan 1:1-7; 2 Fal 24:10-16; 2 Nya 36:10]

8Ndipo Hezekia akamwambia Isaya, Neno la BWANA ulilolinena ni jema. Tena akamwambia, Maana alifikiri, kutakuwapo na amani na usalama katika siku zangu mimi.[#1 Sam 3:18]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya