Yeremia 31

Yeremia 31

Mateka warudi kwa shangwe

1Wakati huo, asema BWANA, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu.

2BWANA asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha.[#Hes 10:33]

3BWANA alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.[#Mal 1:2; Kum 11:28]

4Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi.

5Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake.[#Isa 65:21; Amo 9:14]

6Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni, tukaende Sayuni, kwa BWANA, Mungu wetu.[#Isa 2:3; Mik 4:12]

7Maana BWANA asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee BWANA, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli.[#Isa 12:5]

8Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia, na pamoja nao watakuja walio vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na uchungu wa kuzaa; watarudi huko, jeshi kubwa.[#Eze 34:13]

9Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawapitisha kwenye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.[#Zab 126:5; Yer 50:14; Isa 49:10; 63:16; Kut 4:22; Kum 32:6; 1 Nya 29:10; Yer 3:4,19]

10Lisikieni neno la BWANA, enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali; mkaseme, Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.[#Isa 40:11]

11Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.[#Isa 44:23; 49:24]

12Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, wataukimbilia wema wa BWANA, nafaka, na divai, na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng'ombe; na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji; wala hawatahuzunika tena kabisa.[#Hos 3:5; Ufu 7:17; 21:4; Isa 58:11; 35:10]

13Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, na vijana na wazee pamoja; maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.

14Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono, na watu wangu watashiba kwa wema wangu, asema BWANA.

15BWANA asema hivi,[#Mwa 35:16-19; Mt 2:18; Yos 18:25; Ayu 7:21; Omb 5:7]

Sauti imesikiwa Rama,

kilio, na maombolezo mengi,

Raheli akiwalilia watoto wake;

asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako.

16BWANA asema hivi,[#Eze 11:17,18; Hos 1:11]

Zuia sauti yako, usilie,

na macho yako yasitoke machozi;

Maana kazi yako itapata thawabu,

nao watakuja tena toka nchi ya adui;

Ndivyo asemavyo BWANA.

17Tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema BWANA; na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe.

18Hakika nimemsikia Efraimu, akijililia hivi, Umeniadhibu, nami nikaadhibika, kama ndama asiyeizoea nira; unigeuze, nami nitageuka; kwa maana wewe u BWANA, Mungu wangu.[#Zab 85:4; Yer 17:14; Omb 5:21]

19Hakika baada ya kukugeukia kwangu, nilitubu; na baada ya kufundishwa kwangu, nilijipiga pajani; nilitahayarika, naam, nilifadhaika, kwa sababu niliichukua aibu ya ujana wangu.[#Kum 30:2]

20Je! Efraimu siye mwanangu mpendwa? Je! Siye mtoto apendezaye? Maana kila nisemapo neno juu yake, ningali nikimkumbuka sana; kwa sababu hiyo moyo wangu unataabika kwa ajili yake; bila shaka nitamrehemu, asema BWANA.[#Isa 63:15; 57:18; Hos 11:8; 14:4; Mik 7:18]

21Jiwekee alama za njia; jifanyie miti ya kukuongoza; uuelekeze moyo wako kwenye njia kuu, njia ile ile uliyoiendea; rudi tena, Ee bikira wa Israeli, irudie hii miji yako.[#Yer 50:5]

22Utatangatanga hadi lini, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.[#Yer 2:18; 3:6; Hos 4:16]

23BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Watatumia tena neno hili katika nchi ya Yuda, na katika miji yake, nitakapowarudisha mateka yao; BWANA na akubariki, Ee makao ya haki, Ee mlima wa utakatifu.[#Zab 122:5; Isa 1:26; Zek 8:3]

24Na Yuda, na miji yake yote, watakaa humo pamoja; wakulima, nao waendao huku na huko pamoja na makundi yao.

25Kwa maana nimeishibisha roho yenye uchovu, nami nimeiridhisha kila roho yenye huzuni.

26Basi, nikaamka, nikaangalia; na usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.

Adhabu ya kibinafsi

27Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapoipanda nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, mbegu ya mwanadamu na mbegu ya mnyama.[#Hos 2:23]

28Tena itakuwa, kwa kadiri nilivyowaangalia, ili kung'oa, na kubomoa, na kuangusha, na kuangamiza, na kutesa; kwa kadiri iyo hiyo nitawaangalia, ili kujenga, na kupanda, asema BWANA.[#Yer 44:27; 1:10; 24:6; Dan 9:14]

29Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi.[#Eze 18:2]

30Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.[#Gal 6:5]

31Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.[#Yer 32:40; 33:14; Ebr 8:8; Mt 26:28; Mk 14:24; Lk 22:20; 1 Kor 11:25; 2 Kor 3:6; Ebr 8:8-12]

Agano jipya

32Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nilikuwa mume kwao, asema BWANA.[#Yn 1:17; Kum 1:31]

33Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema BWANA; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.[#Yer 32:40; 24:7; 30:22; Zab 40:8; 2 Kor 3:3; Ebr 10:16]

34Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue BWANA; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hadi aliye mkubwa miongoni mwao, asema BWANA; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.[#Isa 54:13; Yn 6:45; 1 Kor 2:10; Yer 33:8; Rum 11:27; Ebr 10:17]

35BWANA asema hivi, awapaye watu jua, ili kuwa nuru wakati wa mchana, na amri za mwezi na nyota, ili kuwa nuru wakati wa usiku, aichafuaye bahari, hata mawimbi yake yakavuma; BWANA wa majeshi, ndilo jina lake;[#Mwa 1:16; Isa 51:15; Yer 10:16]

36Amri hizi zikiondoka, zisiwe mbele zangu, asema BWANA, ndipo wazao wa Israeli nao wataacha kuwa taifa mbele zangu milele.[#Zab 148:6]

37BWANA asema hivi, Kama mbingu zikiweza kupimwa, na misingi ya dunia ikiweza kugunduliwa huko chini, ndipo wazao wa Israeli pia nitawatupilia mbali, kwa ajili ya hayo yote waliyoyatenda, asema BWANA.[#Yer 33:22]

Yerusalemu utatanuliwa

38Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, mji huu utakapojengwa kwa ajili ya BWANA, toka mnara wa Hananeli hadi katika lango la pembeni.[#Neh 3:1; Zab 69:35; Yer 24:6; Dan 9:25]

39Na kamba ya kupimia itaendelea moja kwa moja hadi katika mlima Garebu, tena itazunguka na kufika Goa.[#Zek 2:1]

40Na bonde lote la mizoga, na majivu, na mashamba yote mpaka kijito Kidroni, mpaka pembe ya lango la farasi, upande wa mashariki, patakuwa patakatifu kwa BWANA; hapatang'olewa, wala hapatabomolewa, hata milele.[#2 Nya 23:15; Neh 3:28; Yoe 3:17]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya