The chat will start when you send the first message.
1Na Yesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho kwa muda wa siku arubaini nyikani,[#Mt 4:1-11; Mk 1:12,13]
2akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; na zilipotimia, aliona njaa.
3Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.
4Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu.[#Kum 8:3]
5Akampandisha juu, akamwonesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja.
6Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa yeyote kama nipendavyo.
7Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.
8Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.[#Kum 6:13,14]
9Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini;
10kwa maana imeandikwa,[#Zab 91:11,12]
Atakuagizia malaika zake wakulinde;
11na ya kwamba,[#Zab 91:12]
Mikononi mwao watakuchukua,
Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
12Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.[#Kum 6:16]
13Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.[#Ebr 4:15]
14Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akaendea Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando.[#Mt 4:12-17; Mk 1:14,15]
15Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote.
16Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.[#Mt 13:53-58; Mk 6:1-6]
17Akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua kitabu, akapata mahali palipoandikwa,[#Isa 61:1,2; 58:6]
18Roho wa Bwana yu juu yangu,[#Isa 61:1-2]
Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiria maskini Habari Njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao,
Na vipofu kupata kuona tena,
Kuwaacha huru waliosetwa,
19Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.[#Law 25:10]
20Akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.
21Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.
22Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu?[#Yn 6:42]
23Akawaambia, Bila shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe.[#Mt 4:13]
24Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii anayekubaliwa katika nchi yake mwenyewe.[#Yn 4:44]
25Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia katika nchi nzima;[#1 Fal 17:1,9; 18:1; Yak 5:17]
26wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni.[#1 Fal 17:8-16]
27Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu.[#2 Fal 5:1-14]
28Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo.
29Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini;
30lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.
31Akashuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya sabato;[#Mk 1:21-28; #Mt 4:13; Yn 2:12]
32wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo.[#Mt 7:28-29; Yn 7:46]
33Na ndani ya sinagogi mlikuwa na mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu,
34akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu.
35Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka pasipo kumdhuru.
36Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka.
37Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile.
38Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake.[#Mt 8:14-17; Mk 1:29-39]
39Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akainuka, akawatumikia.
40Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya.
41Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo.[#Mt 8:29; Mk 3:11,12]
42Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafutatafuta, na walipomfikia, wakataka kumzuia asiondoke kwao.
43Akawaambia, Imenipasa kuihubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana nilitumwa kwa sababu hiyo.[#Lk 8:1]
44Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya.[#Mt 4:23]