Mathayo 16

Mathayo 16

Kudaiwa kwa ishara

1Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaoneshe ishara itokayo mbinguni.[#Mk 8:11-21; #Mt 12:38; Lk 11:16]

2Akajibu, akawaambia, [Jioni ikifika, mnasema, hali ya anga itakuwa mzuri; kwa kuwa mbingu ni nyekundu.[#Lk 12:54-56]

3Na asubuhi, mnasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mnajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za nyakati hizi hamwezi kuzitambua?][#Mt 11:4]

4Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake.[#Mt 12:39; Lk 11:29; Yon 2:1]

Chachu ya Mafarisayo na Masadukayo

5Nao wanafunzi wakaenda hadi ng'ambo, wakasahau kuchukua mikate.

6Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.[#Lk 12:1]

7Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate.

8Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani haba, kwa sababu hamna mikate?[#Mt 6:30]

9Hamjafahamu bado, wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi mlivyoviokota?[#Mt 14:17-21]

10Wala ile mikate saba kwa watu elfu nne, na makanda mangapi mliyoyaokota?[#Mt 15:34-38]

11Imekuwaje hamkufahamu ya kuwa sikuwaambia kwa sababu ya mkate? Ila jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.

12Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.[#Yn 6:27]

Petro amkiri Yesu kuwa Kristo

13Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?[#Mk 8:27-30; Lk 9:18-21]

14Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.[#Mt 14:1-2; 17:10; Mk 6:14-15; Lk 9:7-8]

15Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.[#Yn 6:68-69]

17Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Baryona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.[#Gal 1:15,16; Mt 17:4,5; #16:17 maana yake ‘mwana wa Yona’.]

18Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.[#Yn 1:42; Efe 2:20]

19Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.[#Mt 18:18; Yn 20:23]

20Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote ya kwamba yeye ndiye Kristo.[#Mt 17:9]

Yesu asema juu ya kufa na kufufuka kwake

21Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.[#Mk 8:31—9:1; Lk 9:22-27; #Mt 12:40; Yn 2:19]

22Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, La hasha! Bwana, hayo hayatakupata.

23Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.

Msalaba na kujikana

24Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.[#Mt 10:38; Lk 14:27]

25Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.[#Mt 10:39; Lk 17:33; Yn 12:25]

26Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kuipoteza nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?[#Mt 4:8]

27Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.[#Mt 25:31; Zab 62:12; Rum 2:6; Yn 5:29; Mit 24:12]

28Amin, nawaambieni, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.[#Mt 10:23]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya