The chat will start when you send the first message.
1Na sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.[#Mk 16:1-10; Lk 24:1-10; Yn 20:1-18]
2Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la ardhi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia.
3Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji.[#Mt 17:2; Mdo 1:10]
4Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.
5Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.
6Hayupo hapa; maana amefufuka kama alivyosema. Njooni, mpatazame mahali alipolazwa.[#Mt 12:40; 16:21; 17:23; 20:19; Mdo 2:36]
7Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.[#Mt 26:32]
8Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari.
9Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia.
10Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; nendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.[#Ebr 2:11; Mwa 45:4; 50:19]
11Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya walinzi waliingia mjini, wakawaambia wakuu wa makuhani juu ya mambo yote yaliyotendeka.
12Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi,
13wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala.[#Mt 27:64]
14Na jambo hili likisikika kwa mtawala, sisi tutasema naye, nanyi hamtapata shida.
15Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.
16Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya hadi katika mlima ule aliowaagiza Yesu.[#Mt 26:32; Mk 14:28; Mt 28:7]
17Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao walikuwa na mashaka.
18Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.[#Mt 11:27; Efe 1:20-22; Dan 7:14]
19Basi, nendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;[#Mdo 1:8; Mk 16:15,16]
20na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.[#Mt 18:20; Yn 14:23]