Marko 1

Marko 1

Mahubiri ya Yohana Mbatizaji

1Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya,[#Mal 3:1; Mt 11:10; Yn 3:28]

Tazama, namtuma mjumbe wangu

Mbele ya uso wako,

Atakayeitengeneza njia yako.

3Sauti ya mtu aliaye nyikani,[#Isa 40:3]

Itengenezeni njia ya Bwana,

Yanyosheni mapito yake.

4Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.

5Wakamwendea nchi yote ya Yudea, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.

6Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwituni.[#2 Fal 1:8; Zek 13:4]

7Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake.[#Mdo 13:25]

8Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.

Kubatizwa kwa Yesu

9Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani.[#Lk 2:51; #Mt 3:13-17; Lk 3:21-22; Yn 1:31-34]

10Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake;

11na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.[#Mwa 22:2; Zab 2:7; Isa 42:1; Mt 3:17; 12:18; Mk 9:7; Lk 3:22]

Kujaribiwa kwa Yesu

12Mara Roho akamtoa aende nyikani.[#Mt 4:1-11; Lk 4:1-13]

13Akawako huko jangwani siku arubaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwituni, na malaika walikuwa wakimhudumia.[#Zab 91:13; Yn 1:51]

Mwanzo wa huduma katika Galilaya

14Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu,[#Mt 4:12-17; Lk 4:14,15]

15akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.[#Mt 3:2; Gal 4:4]

Yesu awaita wanafunzi wa kwanza

16Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi.[#Mt 4:18-22; Lk 5:1-11]

17Yesu akawaambia, Njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.[#Mt 13:47]

18Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

19Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa katika mashua, wakizitengeneza nyavu zao.

20Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya mashua pamoja na wafanya kazi wakaenda, wakamfuata.

Mtu mwenye pepo mchafu

21Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha.[#Lk 4:31-37; #Mt 4:13]

22Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama waandishi.[#Mt 7:28,29]

23Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti,

24akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza?[#Mk 5:7; Zab 16:10]

25Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke.

26Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka.[#Mk 9:26]

27Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!

28Habari zake zikaenea haraka kote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.

Yesu awaponya wengi katika nyumba ya Simoni

29Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana.[#Mt 8:14-16; Lk 4:38-41]

30Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, akiugua homa; na mara wakamwambia habari zake.

31Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.

32Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa wagonjwa, na wenye pepo.

33Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni.

34Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.[#Lk 4:41; Mdo 16:17,18]

Yesu ahubiri katika Galilaya

35Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko.[#Lk 4:42-44]

36Simoni na wenziwe wakamfuata;

37nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta.

38Akawaambia, Twendeni mahali pengine, katika vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana nilikuja kwa ajili ya hilo.

39Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.[#Mt 4:23; 9:35]

Yesu amtakasa mtu mwenye ukoma

40Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.[#Mt 8:2-4; Lk 5:12-16]

41Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.

42Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.

43Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara,[#Mk 3:12; 7:36]

44akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila nenda zako ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa ajili ya kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.[#Law 14:1-32; Law 13:49]

45Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini waziwazi; bali alikaa nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila upande.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya