Hesabu 16

Hesabu 16

Uhasama wa Kora, Dathani na Abiramu

1Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni;[#Yud 1:11]

2nao, pamoja na watu kadhaa wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa;[#Hes 26:9]

3nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yuko kati yao; ya nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA?[#Zab 106:16; Kut 19:6; 29:45]

4Musa aliposikia maneno haya, akaanguka kifudifudi;[#Hes 20:6]

5kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi BWANA ataonesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake.[#2 Tim 2:19; Law 21:6-12; Kut 28:1; 1 Sam 2:28; Zab 105:26; Law 10:3; Eze 40:46]

6Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote;

7vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za BWANA kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu atakayechaguliwa na BWANA, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi.

8Musa akamwambia Kora, Sikilizeni basi, enyi Wana wa Lawi;

9Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mhudumu katika maskani ya BWANA, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia;[#1 Sam 18:23; Isa 7:13; Kum 10:8]

10tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia?

11Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha BWANA; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia?[#Kut 16:8; 1 Kor 3:5]

12Kisha Musa akatuma ujumbe wa kuwaita Dathani na Abiramu wana wa Eliabu; nao wakasema, “Hatuji sisi”;

13je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyobubujika na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa?[#Kut 2:14; Mdo 7:27,35]

14Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji.[#Kut 3:8; Law 20:24]

15Musa akakasirika sana, akamwambia BWANA. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao.[#Mwa 4:4,5; 1 Sam 12:3; Mdo 20:33; 2 Kor 7:2]

16Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote kuweni hapa mbele ya BWANA kesho, wewe, na wao, na Haruni;

17mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za BWANA, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake.

18Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni.

19Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa BWANA ukatokea mbele ya mkutano wote.[#Kut 16:7,10; Law 9:6,23]

20Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

21Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja.[#Mwa 19:17; Yer 51:6; Mdo 2:40; Ufu 18:4; Kut 32:10; 33:5; Zab 73:19; Isa 37:36]

22Nao wakaanguka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote?[#Ayu 12:10; Mhu 12:7; Isa 57:16; Zek 12:1; Ebr 12:9; 2 Sam 24:17; 1 Nya 21:17; Eze 18:20]

23BWANA akasema na Musa, na kumwambia,

24Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu.

25Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakafuatana naye.

26Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao chochote, msiangamizwe katika dhambi zao zote.[#Mwa 19:12; Isa 52:11; Mdo 2:40; 2 Kor 6:17; Ufu 18:4]

27Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo.[#Ayu 9:4; Mit 16:18]

28Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba BWANA amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe.[#Kut 3:12; Kum 18:22; Zek 2:9; Yer 23:16; Eze 13:17; Yn 5:30]

29Kama watu hawa wakifa kifo cha kawaida, kama watu wote wafavyo, au kama wataadhibiwa kwa adhabu ya watu wote; hapo basi BWANA hakunituma mimi.[#Kut 20:5; 32:34; Ayu 35:15; Isa 10:3; Yer 5:9; Omb 4:22]

30Lakini BWANA akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao wakashuka shimoni wakiwa hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau BWANA[#Ayu 31:3; Isa 28:21; Zab 55:15; Ufu 9:2]

31Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka;[#Hes 26:10; 27:3; Kum 11:6; Zab 106:17]

32nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote.[#1 Nya 6:22]

33Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wakiwa hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni.

34Nao Israeli wote waliokuwa kandokando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi.

35Kisha moto ukatoka kwa BWANA, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba.[#Hes 11:1; Law 10:2; Zab 106:18]

36Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

37Mwambie Eleazari mwana wa Haruni kuhani, avitoe vile vyetezo hapo penye moto ukaumwage huo moto kule; kwani ni vitakatifu;

38vile vyetezo vya hao waliofanya dhambi na kuziumiza nafsi zao wenyewe, na vifanywe mbao za kufuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu; kwa kuwa walivisongeza mbele za BWANA, navyo ni vitakatifu; vitakuwa ishara kwa wana wa Israeli.[#Mit 20:2; Hab 2:10; Hes 17:10; 26:10; Eze 14:8; 1 Kor 10:11; 2 Pet 2:6]

39Basi Eleazari kuhani akavitwaa vile vyetezo vya shaba, vilivyosongezwa na hao walioteketezwa; nao wakavifua viwe kifuniko cha madhabahu;

40viwe ukumbusho kwa wana wa Israeli, ili mgeni yeyote asiye wa kizazi cha Haruni, asikaribie kufukiza uvumba mbele za BWANA; asiwe mfano wa Kora, na mkutano wake; kama BWANA alivyonena naye, kwa kupitia kwa Musa.[#Hes 3:38; 18:4-7; 1 Fal 13:1]

41Lakini siku ya pili yake mkutano wote wa wana wa Israeli wakamnung'unikia Musa, na Haruni, wakasema, Ninyi mmewaua watu wa BWANA.[#Hes 14:2; Zab 106:13,26; Mt 5:11; Mdo 21:28; 2 Kor 6:8]

42Basi ilikuwa, hapo huo mkutano ulipokuwa umekutanika kinyume cha Musa, na kinyume cha Haruni, wakaangalia upande wa hema ya kukutania; na tazama, hilo wingu likaifunika hema, na utukufu wa BWANA ukaonekana.[#Kut 16:7,10; 24:16; 40:34; Law 9:23; Hes 14:10]

43Na Musa na Haruni wakaenda hapo mbele ya hema ya kukutania.

44Naye BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

45Ondokeni kati ya mkutano, ili niwaangamize mara moja. Wao wakaanguka kifudifudi.[#Hes 20:6; 1 Nya 21:16; Mt 26:39]

46Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, uende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu imetoka kwa BWANA; hiyo tauni imeanza.[#Law 10:6; Hes 1:53; 11:33; 18:5; Yos 7:1; 22:18; 1 Sam 6:19; 2 Sam 24:1; Zab 106:29; 1 Nya 27:24]

47Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu.

48Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wangali hai; tauni ikazuiwa.[#2 Sam 24:16,17,25; Ayu 33:24; Zab 106:30; Mt 20:28; 1 The 1:10; Ebr 7:24; Yak 5:16]

49Basi waliokufa kwa tauni walikuwa elfu kumi na nne na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora.

50Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya