Hesabu 8

Hesabu 8

Taa saba

1Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,[#Kut 25:31-40; 37:17-24]

2Nena na Haruni, ukamwambie, Utakapoziweka taa, hizo taa saba zitatoa nuru hapo mbele ya kinara cha taa.[#Kut 40:25; Law 24:1,2; Zab 119:105; Isa 8:20; Mt 5:14; Yn 1:9; 8:12]

3Basi Haruni akafanya; akaziweka taa zake ili zitoe nuru hapo mbele ya kinara, kama BWANA alivyomwagiza Musa.

4Na hii ndiyo kazi ya hicho kinara cha taa, ilikuwa ni kazi ya ufuzi wa dhahabu; tangu kitako chake hata maua yake kilikuwa ni kazi ya ufuzi; vile vile kama ule mfano BWANA aliokuwa amemwonesha Musa, ndivyo alivyokifanya kinara.[#Kut 25:18,31,40]

Kuwekwa wakfu na huduma ya Walawi

5Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

6Watwae Walawi na kuwaondoa kati ya wana wa Israeli, kisha uwatakase.[#Zab 26:6; Isa 52:11; Ebr 7:26; 10:22]

7Nawe utawafanyia mambo haya ili kuwatakasa; nyunyiza juu yao maji yatakasayo dhambi, nao wajinyoe kwa wembe mwili wote, kisha wazifue nguo zao, na kujitakasa.[#Law 14:8,9]

8Kisha na watwae ng'ombe dume mmoja mchanga, na sadaka yake ya unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, nawe utatwaa ng'ombe dume mchanga mwingine kuwa sadaka ya dhambi.[#Law 2:1]

9Nawe utawaleta Walawi mbele ya hema ya kukutania; nawe utauitisha mkutano wote wa wana wa Israeli;[#Kut 29:4; 40:12; Law 8:3]

10nawe utawaleta Walawi mbele za BWANA; kisha wana wa Israeli wataweka mikono yao juu ya Walawi;[#Law 1:4]

11naye Haruni atawasongeza Walawi mbele za BWANA wawe sadaka ya kutikiswa, kwa ajili ya wana wa Israeli, ili wawe watumishi wa BWANA.

12Kisha Walawi wataweka mikono yao juu ya vichwa vya hao ng'ombe; nawe umtoe mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa BWANA, na huyo wa pili awe sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi.[#Kut 29:10; Law 1:4; 8:14]

13Kisha utawaweka Walawi mbele ya Haruni, na mbele ya wanawe na kuwasongeza kwa BWANA wawe sadaka ya kutikiswa.

14Ndivyo utakavyowatenga Walawi na kuwatoa katika wana wa Israeli; na Walawi watakuwa wangu.[#Hes 3:45; 16:9; Mal 3:17]

15Kisha baadaye Walawi wataingia ndani, ili wahudumu katika hema ya kukutania; nawe utawatakasa, na kuwasongeza wawe sadaka ya kutikiswa.[#Kut 29:24]

16Kwa kuwa nimepewa kabisa mimi watu hawa kutoka katika wana wa Israeli; badala ya wote wafunguao mimba, maana, wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli wote, nimewatwaa wawe wangu.[#Hes 3:12,45]

17Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli ni wangu, wa wanadamu na wa wanyama; siku hiyo niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri niliwatakasa kwa ajili yangu mwenyewe.[#Kut 13:2,12-15; Lk 2:23; Hes 3:13]

18Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote walio katika wana wa Israeli.

19Nami nimempa Haruni hao Walawi wawe kipawa chake yeye na wanawe, kutoka kwa wana wa Israeli, ili wafanye kazi ya kutumikia wana wa Israeli katika hema ya kukutania, kisha wafanye upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli; ili kusiwe na maradhi kati ya wana wa Israeli, hapo wana wa Israeli watakapopakaribia mahali patakatifu.[#Hes 3:9; 18:2-6; 1:53; 16:46; 18:5]

20Basi Musa na Haruni, na mkutano wote wa wana wa Israeli, wakawafanyia Walawi mambo hayo; kama hayo yote BWANA aliyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo wana wa Israeli walivyowafanyia.

21Walawi wakajitakasa na dhambi, nao wakafua nguo zao; kisha Haruni akawasongeza mbele za BWANA wawe sadaka ya kutikiswa; Haruni akafanya kwa ajili yao ili kuwatakasa.[#Rum 15:16]

22Kisha baada ya hayo Walawi wakaingia ili wafanye kazi zao ndani ya hema ya kukutania mbele ya Haruni na mbele ya wanawe; kama BWANA alivyomwagiza Musa kuhusu hao Walawi, ndivyo walivyowafanyia.[#2 Nya 30:15; 31:2]

23Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

24Mambo yawapasayo hao Walawi ni haya; tangu waliopata umri wa miaka ishirini na mitano na zaidi wataingia ndani ili wahudumu katika hema ya kukutania;[#Hes 4:3; 1 Nya 23:3; 24:27]

25tena tangu waliopata umri wa miaka hamsini wasiendelee kuhudumu tena;

26lakini watawasaidia na ndugu zao katika hema ya kukutania, kufanya kazi zao, lakini wasitumike katika huo utumishi tena. Ndivyo utakavyowafanyia Walawi katika mambo ya ulinzi wao.[#Hes 1:53; 1 Nya 23:28-32; 26:20-29; Eze 44:8,11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya