The chat will start when you send the first message.
1Mwanangu, usiisahau sheria yangu,[#Kum 30:16]
Bali moyo wako uzishike amri zangu.
2Maana zitakuongezea wingi wa siku.
Na miaka ya uzima, na amani.
3Rehema na kweli zisiachane nawe;[#Kum 6:8; Yer 17:1; 2 Kor 3:3]
Zifunge shingoni mwako;
Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.
4Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri,[#Lk 2:52; 1 Sam 2:26; Mdo 2:47]
Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.
5Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote,[#Yer 9:23]
Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6Katika njia zako zote mkiri yeye,[#1 Nya 28:9; Yer 10:23]
Naye atayanyosha mapito yako.
7Usiwe na hekima machoni pako;[#Rum 12:16]
Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.
8Itakuwa afya mwilini pako,[#3:8 Au, kitovuni pako.]
Na mafuta mifupani mwako.
9Mheshimu BWANA kwa mali yako,[#Kut 23:19]
Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi,[#Kum 28:8]
Na vyombo vyako vitafurika divai mpya.
11Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na BWANA,[#Ayu 5:17; Ebr 12:5]
Wala usione ni taabu kurudiwa naye.
12Kwa kuwa BWANA ampendaye humrudi,[#Ufu 3:19; Kum 8:5]
Kama vile baba mwanawe ampendezaye.
13Heri mtu yule aonaye hekima,
Na mtu yule apataye ufahamu.
14Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha,[#Ayu 28:13; Mit 2:4; 8:11,19]
Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi.
15Yeye ana thamani kuliko marijani,[#Mt 13:44]
Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.
16Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kulia,[#1 Tim 4:8]
Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.
17Njia zake ni njia za kupendeza sana,[#Mt 11:29]
Na mapito yake yote ni amani.
18Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana;[#Mwa 2:9]
Ana heri kila mtu anayeshikamana naye.
19Kwa hekima BWANA aliiweka misingi ya nchi;[#Mit 8:27; Yn 1:3; Ebr 1:2]
Kwa akili zake akazifanya mbingu imara;
20Kwa maarifa yake vilindi viligawanyika;[#Kum 33:28; Ayu 36:28]
Na mawingu yadondoza umande.
21Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako,
Shika hekima kamili na busara.
22Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako,
Na neema shingoni mwako.
23Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama,
Wala mguu wako hautakwaa.
24Ulalapo hutaona hofu;[#Law 26:6]
Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu.
25Usiogope hofu ya ghafla,
Wala uharibifu wa waovu utakapofika.
26Kwa kuwa BWANA atakuwa tumaini lako,
Naye atakulinda mguu wako usinaswe.
27Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao,[#Rum 13:7; Gal 6:10]
Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.
28Usimwambie jirani yako,[#Law 19:13; Kum 24:15]
Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa;
Nawe unacho kitu kile karibu nawe.
29Usiwaze mabaya juu ya jirani yako,
Ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama.
30Usishindane na mtu bila sababu,[#Rum 12:18]
Ikiwa hakukudhuru kwa lolote.
31Usimhusudu mtu mwenye ujeuri,
Wala usiichague mojawapo ya njia zake.
32Maana mtu mjeuri ni chukizo kwa BWANA,
Bali siri yake ni pamoja na wanyofu.
33Laana ya BWANA i katika nyumba ya waovu,[#Zek 5:4; Mal 2:2; Zab 1:3]
Bali huibariki maskani ya mwenye haki.
34Hakika yake huwadharau wenye dharau,[#Yak 4:6; 1 Pet 5:5; Zab 138:6; Mt 23:12]
Bali huwapa wanyenyekevu neema.
35Wenye hekima wataurithi utukufu,[#Dan 12:2]
Bali kukuzwa kwa wapumbavu ni fedheha.