Zaburi 101

Zaburi 101

Ahadi ya mfalme juu ya uaminifu na haki

1Rehema na hukumu nitaziimba,

Ee BWANA, nitakuimbia zaburi.

2Nitakuwa na mwenendo usio na hatia;[#1 Sam 18:14; Mwa 18:19; Kum 6:7; 1 Fal 9:4]

Utakuja kwangu lini?

Nitakwenda kwa unyofu wa moyo

Ndani ya nyumba yangu.

3Sitaweka mbele ya macho yangu[#Yos 23:6; 1 Sam 12:20]

Neno la uovu.

Kazi yao waliopotoka naichukia,

Haitaambatana nami.

4Moyo wa ukaidi utaondoka kwangu,[#Mt 7:23; 1 Kor 5:11; 2 Tim 2:19]

Lililo ovu sitalijua.

5Amsingiziaye jirani yake kwa siri,[#Mit 6:17; Lk 18:14]

Huyo nitamwangamiza.

Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno,

Huyo sitamvumilia.

6Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi,[#Rum 13:4]

Hao wakae nami.

Yeye aendaye katika njia kamilifu,

Ndiye atakayenitumikia.

7Hatakaa ndani ya nyumba yangu

Mtu atendaye hila.

Asemaye uongo hatathibitika

Mbele ya macho yangu.

8Kila asubuhi nitawaangamiza[#Yer 21:12; Hos 9:3]

Waovu wote nchini.

Nikiwatenga wote watendao uovu

Na mji wa BWANA.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya