Zaburi 119

Zaburi 119

Utukufu wa sheria ya Mungu

1Heri walio kamili njia zao,[#Zab 128:1]

Waendao katika sheria ya BWANA.

2Heri wazitiio shuhuda zake,[#Kum 4:29]

Wamtafutao kwa moyo wote.

3Naam, hawakutenda ubatili,[#Rum 7:16,17; 1 Yoh 3:9]

Wamekwenda katika njia zake.

4Wewe umetuamuru mausia yako,

Ili sisi tuyatii sana.

5Ningependa njia zangu ziwe thabiti,[#Yer 31:33; Rum 7:22,23; 2 Kor 3:5]

Nizitii amri zako.

6Ndipo mimi sitaaibika,[#Ayu 22:26; 1 Yoh 2:28]

Nikiyaangalia maagizo yako yote.

7Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,

Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako.

8Nitazitii amri zako,

Usiniache kabisa.

* * *

9Jinsi gani kijana aisafishe njia yake?[#Mit 1:4,10]

Kwa kutii, akilifuata neno lako.

10Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,[#2 Nya 15:15]

Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.

11Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,[#Lk 2:19]

Nisije nikakutenda dhambi.

12Ee BWANA, umehimidiwa,

Unifundishe amri zako.

13Kwa midomo yangu nimezisimulia

Hukumu zote za kinywa chako.

14Nimeifurahia njia ya shuhuda zako

Kana kwamba ni mali mengi.

15Nitayatafakari maagizo yako,[#Zab 1:2]

Na kuziangalia njia zako.

16Nitajifurahisha sana kwa amri zako,

Sitalisahau neno lako.

* * *

17Umtendee mtumishi wako ukarimu,

Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.

18Unifumbue macho yangu niyatazame

Maajabu yatokayo katika sheria yako.

19Mimi ni mgeni katika nchi,[#Mwa 47:9; Ebr 11:13]

Usinifiche maagizo yako.

20Roho yangu imepondeka kwa kutamani

Hukumu zako kila wakati.

21Umewakemea wenye kiburi,

Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.

22Uniondolee laumu na dharau,

Kwa maana nimezishika shuhuda zako.

23Wakuu nao waliketi wakaninena,

Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.

24Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,

Na washauri wangu.

* * *

25Nafsi yangu imegandamia mavumbini,[#Zab 143:11]

Unihuishe sawasawa na neno lako.

26Nilizisimulia njia zangu ukanijibu,[#1 Fal 8:36; Zab 27:11]

Unifundishe amri zako.

27Unifahamishe njia ya maagizo yako,

Nami nitayatafakari maajabu yako.

28Nafsi yangu imeyeyuka kwa huzuni,

Unitie nguvu sawasawa na neno lako.

29Uniondolee njia ya uongo,[#Mit 30:8; Ebr 8:10]

Unineemeshe kwa sheria yako.

30Nimeichagua njia ya uaminifu,

Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.

31Nimeambatana na shuhuda zako,

Ee BWANA, usiniaibishe.

32Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako,[#1 Fal 4:29; Isa 60:5; 2 Kor 6:11]

Utakaponipanulia ufahamu wangu.

* * *

33Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako,[#Mt 10:22; Ufu 2:26]

Nami nitaishika hadi mwisho.

34Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,[#Mit 2:6; Yak 1:5]

Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.

35Uniendeshe katika mapito ya amri zako,

Kwa maana nimependezwa nayo.

36Unielekeze moyo wangu katika shuhuda zako,[#Eze 33:31; Mk 7:21; Lk 12:15; 1 Tim 6:10; Ebr 13:5]

Wala usiielekee tamaa.

37Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa,[#Ayu 31:1]

Unihuishe katika njia yako.

38Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako,[#2 Sam 7:25]

Iliyo ya wanaokucha.

39Uniondolee laumu niiogopayo,

Maana hukumu zako ni njema.

40Tazama, nimeyatamani mausia yako,

Unihuishe kwa haki yako.

* * *

41Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi,

Naam, wokovu wako kulingana na ahadi yako.

42Nami nitamjibu neno anilaumuye,

Kwa maana nilitumainia neno lako.

43Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe,

Maana nimezingojea hukumu zako.

44Nami nitaitii sheria yako daima,

Naam, milele na milele.

45Nami nitakwenda kwa uhuru,[#Yn 8:32,36; Rum 8:2]

Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.

46Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme,[#Mt 10:18; Mdo 26:1,2]

Wala sitaona aibu.

47Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako,

Ambayo nimeyapenda.

48Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda,

Nami nitazitafakari amri zako.

* * *

49Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako,

Ambalo kwalo umenipa tumaini.

50Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu,[#Zab 27:13; Yer 15:16; Rum 5:3-5; Ebr 6:17-19]

Ya kwamba ahadi yako imenipa moyo.

51Wenye kiburi wamenidharau mno,[#Yer 20:7; Ayu 23:11]

Lakini sikiuki sheria zako.

52Ninapozikumbuka hukumu zako za tangu kale,

Ee BWANA, ninafarijika.

53Ghadhabu kuu imenishika kwa sababu ya wasio haki,[#Ezr 9:3]

Waiachao sheria yako.

54Amri zako zimekuwa nyimbo zangu,

Katika nyumba yangu ya ugenini.

55Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako,[#Zab 63:6]

Ee BWANA, nikaitii sheria yako.

56Hayo ndiyo niliyokuwa nayo,

Kwa sababu nimeyashika mausia yako.

* * *

57BWANA ndiye aliye fungu langu,[#Zab 16:5; Yer 10:16; Omb 3:24]

Ninaahidi kuyatii maneno yake.

58Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote,

Unifadhili kulingana na ahadi yako.

59Ninapozitafakari njia zako,[#Omb 3:40; Yoe 2:13; Lk 15:17]

Naielekeza miguu yangu kwa shuhuda zako.

60Nilifanya haraka wala sikukawia,

Kuyatii maagizo yako.

61Japo kamba za wasio haki zimenifunga,

Siisahau sheria yako.

62Usiku wa manane nitaamka nikushukuru,[#Mdo 16:25]

Kwa sababu ya hukumu zako za haki.

63Mimi ni mwenzi wa watu wote wakuchao,

Na wale wayatiio mausia yako.

64BWANA, dunia imejaa fadhili zako,[#Zab 33:5]

Unifundishe amri zako.

* * *

65Umemtendea mtumishi wako mema,

Ee BWANA, sawasawa na neno lako.

66Unifundishe akili na maarifa,

Maana nimeyaamini maagizo yako.

67Kabla sijateswa mimi nilipotea,[#Kum 32:15; Yer 31:18; Hos 5:15; Ebr 12:11; Ufu 3:19]

Lakini sasa nimelitii neno lako.

68Wewe U mwema na mtenda mema,[#Kut 34:6; Zab 107:1; Mt 19:7]

Unifundishe amri zako.

69Wenye kiburi wamenizulia uongo,[#Ayu 13:4]

Lakini kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako.

70Mioyo yao imenenepa kama shahamu,[#Mdo 28:27]

Lakini mimi nimeifurahia sheria yako.

71Ilikuwa vema kwangu kuwa niliteswa,[#Ebr 12:10; Mit 8:10]

Nipate kujifunza amri zako.

72Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,

Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.

* * *

73Mikono yako iliniumba na kunidhibiti,[#Ayu 10:8; Zab 100:3]

Unifahamishe nikajifunze amri zako.

74Wakuchao na wanione na kufurahi,[#Zab 34:2]

Kwa sababu nimelitumainia neno lako.

75Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,[#Zab 89:30-33; Ebr 12:10]

Ee BWANA, na kwa uaminifu umenitesa.

76Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu,

Kulingana na ahadi yako kwa mtumishi wako.

77Rehema zako zinijie nipate kuishi,

Maana sheria yako ni furaha yangu.

78Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo,[#Zab 25:3]

Mimi nitayatafakari mausia yako.

79Wakuchao na wanirudie,

Nao watazijua shuhuda zako.

80Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako,[#2 Nya 15:7; Mit 4:23; Yn 1:47]

Nisije mimi nikaaibika.

* * *

81Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako,[#Zab 42:1,2; 73:26]

Nimelitumainia neno lako.

82Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako,[#Zab 69:3]

Nikisema, Lini utakaponifariji?

83Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi,[#Ayu 30:30]

Sikuzisahau amri zako.

84Siku za mtumishi wako ni ngapi,[#Zab 39:4; 7:6; Ufu 6:10]

Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia?

85Wenye kiburi wamenichimbia mashimo,[#Zab 35:7]

Ambao hawaifuati sheria yako.

86Amri zako zote ni za kudumu,[#Zab 7:1-5; 35:19]

Ninateswa bila sababu, nisaidie!

87Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi,

Lakini sikuyaacha mausia yako.

88Uniponye kwa fadhili zako,

Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.

* * *

89Ee BWANA, neno lako lasimama[#Mt 5:18; 1 Pet 1:25]

Imara mbinguni hata milele.

90Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi,

Umeiweka nchi, nayo imethibitika.

91Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo,[#Mwa 8:22; Zab 148:6; Yer 33:25]

Maana vitu vyote ni watumishi wako.

92Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu,[#Rum 15:4]

Hapo ningalipotea katika mateso yangu.

93Hata milele sitayasahau maagizo yako,

Maana kwa hayo umenihuisha.

94Mimi ni wako, uniokoe,[#Hos 2:7,16]

Kwa maana nimejifunza mausia yako.

95Wasio haki wameniotea ili kunipoteza,

Nitazitafakari shuhuda zako.

96Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho,[#Isa 40:8; Mt 5:18]

Bali amri yako haina kikomo.

* * *

97Sheria yako naipenda mno ajabu,[#Zab 1:2]

Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.

98Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu,[#Kum 4:6,8; Isa 48:17]

Kwa maana ninayo sikuzote.

99Ninazo akili kuliko waalimu wangu wote,[#2 Tim 3:15]

Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.

100Ninao ufahamu kuliko wazee,[#Ayu 12:12; 32:7]

Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.

101Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya,[#2 Kor 7:1; Mit 1:15]

Ili nilitii neno lako.

102Sikuziacha hukumu zako,

Maana Wewe mwenyewe umenifundisha.

103Mausia yako ni matamu sana kwangu,[#Zab 19:10; Mit 8:11]

Kupita asali kinywani mwangu.

104Kwa mausia yako najipatia ufahamu,

Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.

* * *

105Neno lako ni taa ya miguu yangu,

Na mwanga wa njia yangu.

106Nimeapa nami nikathibitisha,[#Neh 10:29]

Kuzishika hukumu zako za haki.

107Nimeteswa mno;

Ee BWANA, unihuishe sawasawa na neno lako.

108Ee BWANA, uziridhie sadaka za kinywa changu,[#Hos 14:2; Ebr 13:15]

Na kunifundisha hukumu zako.

109Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima,[#Amu 12:3; Ayu 13:14]

Lakini sheria yako sikuisahau.

110Watendao uovu wamenitegea mtego,

Lakini sitoki katika njia ya mausia yako.

111Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,[#Kum 33:4]

Maana ndizo changamko la moyo wangu.

112Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako,

Daima, naam, hata milele.

* * *

113Watu wa kusitasita nawachukia,

Lakini sheria yako naipenda.

114Ndiwe sitara yangu na ngao yangu,[#Zab 32:7]

Neno lako nimelingojea.

115Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu,[#Zab 6:8; Mt 7:23]

Niyashike maagizo ya Mungu wangu.

116Unitegemeze kulingana na ahadi yako, nikaishi,[#Zab 25:2; Rum 5:5; 9:33]

Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.

117Unisaidie nami nitakuwa salama,[#Zab 71:6; Yn 10:28; Rum 14:4]

Nami nitaziangalia amri zako daima.

118Umewakataa wote wazikosao amri zako,

Kwa maana hila zao ni bure.

119Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka,[#Eze 22:18]

Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.

120Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe,[#Hab 3:16]

Nami ninaziogopa hukumu zako.

* * *

121Nimefanya hukumu na haki,

Usiniache mikononi mwao wanaonionea.

122Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema,[#Ebr 7:22]

Wenye kiburi wasinionee.

123Macho yangu yanafifia kwa kuungojea wokovu wako,

Na kutimizwa kwa ahadi yako ya haki.

124Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako,

Na amri zako unifundishe.

125Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe,

Nipate kuzijua shuhuda zako.

126Wakati umewadia BWANA atende kazi;

Kwa kuwa wameitangua sheria yako.

127Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako,[#Zab 19:10; Efe 3:8; Mit 3:13,18; 8:11]

Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.

128Maana nayafuata mausia yako yote, kuwa ya adili,

Kila njia ya uongo naichukia.

* * *

129Shuhuda zako ni za ajabu,

Ndiyo maana roho yangu imezishika.

130Kufafanuliwa kwa maneno yako kunatia nuru,[#Zab 19:11; Mit 1:4; 2 Pet 1:19]

Na kumfahamisha mjinga.

131Nafunua kinywa changu nikihema,

Maana nazitamani amri zako.

132Unigeukie na kunirehemu,[#Kut 4:31; 1 Sam 1:11; Zab 106:4]

Kama ilivyo desturi yako kwa walipendalo jina lako.

133Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako,[#Rum 6:12]

Uovu usije ukanimiliki.

134Unikomboe kutoka kwa dhuluma ya mwanadamu,[#Lk 1:74]

Nipate kuyashika mausia yako.

135Umwangazie mtumishi wako uso wako,[#Zab 4:6]

Na kunifundisha amri zako.

136Macho yangu yachuruzika mito ya machozi,[#Yer 9:1]

Kwa sababu hawaitii sheria yako.

* * *

137Ee BWANA, Wewe ndiwe mwenye haki,[#Neh 9:33; Yer 12:1; Dan 9:7]

Na hukumu zako ni za adili.

138Umeziagiza shuhuda zako kwa haki,

Na kwa uaminifu mwingi.

139Juhudi yangu imeniangamiza,

Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako.

140Neno lako limesafika sana,

Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda.

141Mimi ni mdogo, nadharauliwa,[#Mit 15:16; Amo 7:2; Lk 6:20; 2 Kor 8:9; Yak 2:5]

Lakini siyasahau mausia yako.

142Haki yako ni haki ya milele,[#Zab 19:9; Yn 17:17; Efe 1:13]

Na sheria yako ni kweli.

143Taabu na dhiki zimenipata,

Maagizo yako ni furaha yangu.

144Haki ya shuhuda zako ni ya milele,

Unifahamishe, nami nitaishi.

* * *

145Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee BWANA, uitike;

Nitazishika amri zako.

146Nimekuita Wewe, uniokoe,

Nami nitazishika shuhuda zako.

147Naamka kabla ya mapambazuko na kukuomba msaada,

Naweka tumaini langu katika maneno yako.

148Nakaa macho usiku kucha,[#Zab 63:1,6]

Ili kuitafakari ahadi yako.

149Kwa fadhili zako uisikie sauti yangu,

Ee BWANA, uniokoe.

150Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki,

Wamekwenda mbali na sheria yako.

151Ee BWANA, Wewe U karibu,[#Zab 145:18]

Na maagizo yako yote ni kweli.

152Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako,[#Lk 21:33]

Ya kuwa umeziweka zikae milele.

* * *

153Uyaangalie mateso yangu, uniokoe,[#Omb 5:1]

Maana sikuisahau sheria yako.

154Unitetee na kunikomboa,[#1 Sam 24:15; Zab 35:1; Mik 7:9]

Unihuishe sawasawa na ahadi yako.

155Wokovu u mbali na wasio haki,[#Ayu 5:4]

Kwa maana hawajifunzi amri zako.

156Ee BWANA, rehema zako ni nyingi,

Unihuishe sawasawa na hukumu zako.

157Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi,

Lakini mimi sikiuki shuhuda zako.

158Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa,

Kwa sababu hawakulitii neno lako.

159Uangalie niyapendavyo mausia yako,

Ee BWANA, unihuishe sawasawa na fadhili zako.

160Jumla ya neno lako ni kweli,

Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.

* * *

161Wakuu wameniudhi bure,[#1 Sam 24:11]

Ila moyo wangu unakaa kwa kicho cha maneno yako.

162Naifurahia ahadi yako,

Kama apataye mateka mengi.

163Nimeuchukia uongo, umenikirihi,

Sheria yako nimeipenda.

164Mara saba kila siku nakusifu,

Kwa sababu ya hukumu za haki yako.

165Wana amani nyingi waipendao sheria yako,[#Mit 3:2; Isa 32:17]

Wala hawana la kuwakwaza.

166Ee BWANA, nimeungojea wokovu wako,

Na maagizo yako nimeyatenda.

167Nafsi yangu imezishika shuhuda zako,

Nami nazipenda mno.

168Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako,[#Ayu 34:21; Mit 5:21]

Maana njia zangu zote ziko mbele zako.

* * *

169Ee BWANA, kilio changu na kikufikie,

Unifahamishe sawasawa na neno lako.

170Dua yangu na ifike mbele zako,

Uniponye sawasawa na ahadi yako.

171Midomo yangu na itoe sifa,

Kwa kuwa unanifundisha mausia yako.

172Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako,

Maana maagizo yako yote ni ya haki.

173Mkono wako na uwe tayari kunisaidia,[#Yos 24:22; Mit 1:29; Lk 10:42]

Maana nimeyachagua mausia yako.

174Ee BWANA, nimeutamani wokovu wako,

Na sheria yako ndiyo furaha yangu.

175Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu,

Na hukumu zako zinisaidie.

176Nimetangatanga kama kondoo aliyepotea;[#Isa 53:6; Mt 10:6; Lk 15:4; 1 Pet 2:25; Eze 34:6; Mt 18:11]

Umtafute mtumishi wako;

Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya