Zaburi 33

Zaburi 33

Ukuu na wema wa Mungu

1Mpigieni BWANA vigelegele, enyi wenye haki,

Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

2Mshukuruni BWANA kwa kinubi,

Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.

3Mwimbieni wimbo mpya,[#Isa 42:10]

Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.

4Kwa kuwa neno la BWANA lina adili,

Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.

5Huzipenda haki na hukumu,

Nchi imejaa fadhili za BWANA.

6Kwa neno la BWANA mbingu ziliumbwa,[#Yn 1:1-3; Ebr 11:3; Ayu 26:13]

Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.

7Hukusanya maji ya bahari chungu chungu,

Huviweka vilindi katika ghala.

8Nchi yote na imwogope BWANA,

Wote wakaao duniani na wamche.

9Maana Yeye alisema, na ikawa;[#Mwa 1:3]

Na Yeye aliamuru, ikaumbika.

10BWANA huyabatilisha mashauri ya mataifa,

Huitangua mipango ya watu.

11Shauri la BWANA lasimama milele,[#Ayu 23:13; Mit 19:21; Eze 38:10; Mdo 4:27,28]

Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.

12Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao,

Watu aliowachagua kuwa urithi wake.

13Toka mbinguni BWANA huchungulia,[#2 Nya 16:9; Ayu 28:24; Zab 11:4]

Huangalia na kuwaona wanadamu wote.

14Akiwa katika kiti chake cha enzi.

Huwaangalia wote wakaao duniani.

15Yeye aiumbaye mioyo yao wote[#Isa 64:8; Ayu 11:11; Zab 44:21; Mit 24:12; Yer 32:19; Hes 7:2]

Na kuziona kazi zao zote.

16Mfalme haokolewi kwa jeshi lake kubwa,

Wala shujaa haokoki kwa kuwa na nguvu nyingi.

17Farasi hafai kitu kwa wokovu,

Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake.

18Tazama, jicho la BWANA li kwao wamchao,[#Ayu 36:7; Zab 34:15]

Wazingojeao fadhili zake.

19Ili kuwaponya nafsi zao kutoka kwa mauti,

Na kuwahuisha wakati wa njaa.

20Nafsi zetu zinamngoja BWANA;

Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.

21Maana mioyo yetu itamfurahia,

Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.

22Ee BWANA, fadhili zako zikae nasi,

Kama tunavyo kutumainia Wewe.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya