Zaburi 66

Zaburi 66

Sifa kwa ajili ya wema wa Mungu kwa Israeli

1Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,

2Imbeni utukufu wa jina lake,

Tukuzeni sifa zake.

3Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini![#Zab 18:44]

Kwa ajili ya wingi wa nguvu zako,

Adui zako watakuja kunyenyekea mbele zako.

4Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,[#Zab 67:3]

Naam, italiimbia jina lako.

5Njoni myaone matendo ya Mungu;[#Zab 46:8]

Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu;

6Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;[#Kut 14:21; Yos 3:14-17; Zab 78:13; Isa 63:13,14]

Katika mto walivuka kwa miguu;

Huko ndiko tulikomfurahia yeye.

7Atawalaye kwa uweza wake milele;[#Zab 11:4]

Ambaye macho yake yanaangalia mataifa;

Hebu wanaoasi wasijitukuze nafsi zao.

8Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu,

Itangazeni sauti ya sifa zake;

9Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai,

Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe.

10Kwa maana umetupima, Ee Mungu,[#Zek 13:9]

Umetujaribu inavyojaribiwa fedha.

11Ulituingiza ndani ya wavu,

Na kuweka viunoni mwetu mzigo uliotulemea.

12Uliwapandisha watu

Juu ya vichwa vyetu.

Tulipitia motoni na majini;

Ukatutoa na kutuleta kwenye ufanisi.

13Nitaingia nyumbani mwako na kafara;[#Zab 116:14,18; Mhu 5:4; Yon 2:9]

Nitaondoa kwako nadhiri zangu;

14Ambazo midomo yangu ilizinena;

Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni.

15Kafara za vinono nitakutolea,

Pamoja na fukizo la kondoo dume,

Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi.

16Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,

Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.

17Nilimwita kwa kinywa changu,

Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu.

18Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu,[#Ayu 11:14,15; Mit 15:29; Isa 1:15]

Bwana asingesikia.

19Hakika Mungu amesikia;

Ameisikiliza sauti ya maombi yangu.

20Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu,

Wala kuniondolea fadhili zake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya