The chat will start when you send the first message.
1Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli,
Kwa hao walio safi mioyo yao.
2Nami miguu yangu ilikuwa karibu kupotoka,
Hatua zangu zilikuwa karibu kuteleza.
3Maana niliwaonea wivu wenye kujivuna,
Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki.
4Maana hawana maumivu katika kufa kwao,
Na miili yao ina nguvu.
5Hawana taabu kama watu wengine,
Wala hawapati mapigo kama wanadamu wenzao.
6Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao,[#Mhu 8:11]
Udhalimu huwavika kama nguo.
7Macho yao hutokeza kwa kunenepa,
Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao.
8Hudhihaki, husimulia mabaya,[#2 Pet 2:18; Yud 1:16]
Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu.
9Wameweka kinywa chao mbinguni,[#Ufu 13:6]
Na ulimi wao hutangatanga duniani.
10Kwa hiyo watu wake hugeuka huko,
Na maji yaliyojaa humezwa nao.
11Nao husema, Mungu ajuaje?[#Ayu 22:13; Zab 94:7]
Yako maarifa kwake aliye juu?
12Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki,
Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi.
13Hakika nimejisafisha moyo wangu bure,[#Ayu 21:15; Zab 24:4; Mal 3:14; Ebr 10:19-22]
Na kunawa mikono yangu nisitende dhambi.
14Maana mchana kutwa nimepigwa,
Na kuadhibiwa kila asubuhi.
15Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo;
Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako.
16Nami nilifikiri jinsi ya kufahamu hayo;[#Mhu 8:17]
Ikawa taabu machoni pangu;
17Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu,[#Zab 77:13]
Nikautafakari mwisho wao.
18Hakika Wewe huwaweka penye utelezi,
Huwaangusha mpaka palipoharibika.
19Namna gani wameangamizwa punde!
Wakafutiliwa mbali kwa vitisho.
20Ee Bwana, wamekuwa kama ndoto wakati wa kuamka,
Uondokapo utaidharau sanamu yao.
21Moyo wangu ulipoona uchungu,
Viuno vyangu viliponichoma,
22Nilikuwa kama mjinga, sijui neno;
Nilikuwa kama mnyama tu mbele zako.
23Walakini mimi ni pamoja nawe daima,
Umenishika mkono wa kulia.
24Utaniongoza kwa shauri lako,[#Isa 58:8; Yn 14:3; 2 Kor 5:1]
Na baadaye utanikaribisha kwa utukufu.
25Ni nani niliye naye mbinguni,[#Isa 26:8,9; Hab 3:17,18]
Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe.
26Mwili wangu na moyo wangu hupunguka,[#Zab 84:2]
Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu
Na sehemu yangu milele.
27Maana wajitengao nawe watapotea;
Umewaangamiza wote waliokuacha Wewe.
28Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu;[#Ebr 10:22]
Nimefanya kimbilio kwa Bwana MUNGU,
Niyahubiri matendo yako yote.