Zaburi 75

Zaburi 75

Shukrani kwa wema aliotenda Mungu

1Ee Mungu, tunakushukuru.

Tunakushukuru kwa kuwa Jina lako liko karibu;

Watu huyasimulia matendo yako ya ajabu.

2Nitakapoufikia wakati ulioamriwa,

Mimi nitahukumu hukumu za haki.

3Ingawa dunia na wote wakaao humo wataharuki,[#Ebr 1:3]

Mimi mwenyewe nimezisimamisha nguzo zake.

4Niliwaambia waliojivuna, Msijivune;

Na wasio haki, Msiiinue pembe.

5Msiiinue pembe yenu juu,

Wala msinene kwa shingo ya kiburi.

6Maana siko mashariki wala magharibi,

Wala nyikani itokako heshima.

7Bali Mungu ndiye ahukumuye;[#1 Sam 2:7; 2 Sam 5:2; Dan 2:21; Lk 1:52]

Humdhili huyu na kumwinua huyu.

8Maana mkononi mwa BWANA mna kikombe,[#Ayu 21:20; Yer 25:15; Ufu 14:10]

Na mvinyo yake inatoka povu;

Kumejaa machanganyiko;

Naye huyamimina.

Na sira zake wasio haki wa dunia

Watazifyonza na kuzinywa.

9Bali mimi nitatangaza matendo yako milele,

Nitamwimbia Mungu wa Yakobo.

10Nguvu zote za wasio haki nitazimaliza,

Lakini nguvu za mwenye haki nitaziimarisha.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya