The chat will start when you send the first message.
1Nimpazie Mungu sauti yangu,
Naam, nimpazie Mungu, naye atanisikia.
2Katika siku ya taabu yangu nilimtafuta Bwana;[#Zab 50:15; Isa 26:9]
Mkono wangu ulinyoshwa usiku, bila kulegea;
Nafsi yangu ilikataa kufarijika.
3Nilipotaka kumkumbuka Mungu nilifadhaika;
Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia.
4Ulizishika kope za macho yangu zisifumbike;
Nilitaabika nisiweze kunena.
5Nilifikiri habari za siku za kale,[#Kum 32:7; Zab 14:5; Isa 51:9]
Miaka ya zamani zilizopita.
6Nanena na moyo wangu usiku,
Nawaza moyoni mwangu,
Roho yangu naipeleleza.
7Je! Bwana atatutupa milele na milele?
Asiwe na fadhili kwetu kamwe?
8Rehema zake zimekoma hata milele?[#Isa 27:11; Yon 2:4; Hes 23:19; Yer 15:18; Rum 9:6]
Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote?
9Mungu amesahau fadhili zake?[#Isa 49:15]
Amezuia kwa hasira rehema zake?
10Nikasema, Ndio udhaifu wangu huo;[#Ayu 42:3; Zab 31:22; Yer 10:19]
Lakini nitaikumbuka miaka ya mkono wa kulia wake Aliye Juu.
11Nitayakumbuka matendo ya BWANA;[#1 Nya 16:12; Zab 28:5; Isa 5:1]
Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale.
12Pia nitaitafakari kazi yako yote;
Nitaziwaza habari za matendo yako.
13Ee Mungu, njia yako iko katika utakatifu;[#Zab 73:17]
Ni Mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu?
14Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu;
Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa.
15Kwa mkono wako umewakomboa watu wako,
Wana wa Yakobo na Yusufu.
16Ee Mungu, yale maji yalikuona,[#Kut 14:21; Yos 3:15,16]
Yale maji yalikuona, yakaogopa.
Vilindi vya maji navyo vikatetemeka,
17Mawingu yakamwaga maji.
Mbingu nazo zikatoa sauti,
Mishale yako nayo ikatapakaa.
18Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli;
Umeme uliuangaza ulimwengu.
Nchi ilitetemeka na kutikisika;
19Njia yako ilikuwa katika bahari.[#Hab 3:15; Kut 14:28; Ayu 37:23]
Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu;
Hatua zako hazikujulikana.
20Uliwaongoza watu wako kama kundi,[#Isa 63:11]
Kwa mkono wa Musa na Haruni.