Zaburi 81

Zaburi 81

Ombi la Mungu kwa Waisraeli wakaidi

1Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha,

Mshangilieni Mungu wa Yakobo.

2Pazeni zaburi, pigeni matari,

Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda.

3Pigeni panda mwandamo wa mwezi,[#Hes 10:10]

Kukiwa na mbalamwezi, wakati wa sikukuu yetu.

4Kwa maana ni sheria kwa Israeli,[#Law 23:24; Hes 10:10]

Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo.

5Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu,

Alipoondoka juu ya nchi ya Misri;

Maneno yake nisiyemjua niliyasikia.

6Nimeutua mzigo begani mwake;

Mikono yake nikaiondolea kazi nzito.

7Katika shida uliniita nikakuokoa;[#Kut 17:7; Hes 20:13]

Nilikuitikia kutoka maficho yangu ya radi;

Nilikujaribu penye maji ya Meriba.

8Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya,

Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza;

9Usiwe na mungu mgeni ndani yako;[#Kut 20:2-3; Kum 5:6-7]

Wala usimsujudie mungu mwingine.

10Mimi ndimi BWANA, Mungu wako,[#Zab 37:3; Yn 15:7]

Niliyekupandisha toka nchi ya Misri;

Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.

11Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu,

Wala Israeli hawakunitaka.

12Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao,[#Mdo 7:42; Rum 1:24]

Waenende katika mashauri yao.

13Laiti watu wangu wangenisikiliza,[#Kum 5:29; Isa 48:18; Yer 44:4,5; Mt 23:37]

Na Israeli angeenenda katika njia zangu;

14Ningewadhili adui zao kwa upesi,

Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu;

15Wamchukiao BWANA wangenyenyekea mbele zake,

Na maangamizi yao yangedumu milele.

16Naam, ningewalisha kwa ngano iliyo bora zaidi,

Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya