Yoshua Mwana wa Sira 24

Yoshua Mwana wa Sira 24

Hutuba ya Hekima

1Hekima atajisifu nafsi yake, na katikati ya watu wake atajiadhimisha;

2katika mkutano wa Aliye Juu atafumbua kinywa chake na kujitukuza mbele ya majeshi yake.

3Mimi nilitoka kinywani mwake Aliye Juu,

Na kama ukungu nikaifunikiza nchi.

4Nikafanya maskani yangu palipo juu,[#Kut 33:9-10]

Na kiti changu katika nguzo ya wingu.

5Mviringo wa mbingu nikauzunguka peke yangu,

Nikatembea katika vilindi vya bahari.

6Katika mawimbi ya bahari, na duniani pote,

Katika kila taifa na kabila nikamiliki.

7Pamoja na hao wote nikatafuta kikao;

Na nipate kituo katika urithi wa nani?

8Ndipo Muumba vitu vyote aliponiagiza,

Aliyeniumba aliisimamisha hema yangu;

Akasema, Maskani yako iwe katika Yakobo,

Urithi wako na uwe katika Israeli.

9Tangu awali aliniumba kabla ya ulimwengu,

Wala sikomi kabisa hata milele.

10Katika Hema Takatifu nikahudumu mbele zake,

Vivyo hivyo nikathibitika katika Sayuni.

11Katika mji upendwao akanistarehesha,

Na katika Yerusalemu nikapewa amri;

12Nikatia shina katika taifa lililo tukufu,

Naam, katika sehemu ya urithi wa BWANA.

13Nikakuzwa kama mwerezi wa Lebanoni,

Kama mshemeni milimani pa Hermoni.

14Nikakuzwa kama mtende uotao pwani,

Mithili ya miwaridi penye Yeriko.

Kama mzeituni mzuri katika uwanda,

Na kama mwaramoni nikakuzwa.

15Kama mdalasini na mdewere na manemane

Nikatapanya harufu ya kupendeza;

Mithili ya uudi na unuka na ubani,

Na kama moshi wa uvumba hekaluni.

16Kama mweloni nikanyosha matawi yangu,

Na matawi yangu yana utukufu na uzuri.

17Kama mzabibu nikachipuza neema,

18Na maua yangu ni matunda ya ukwasi,

19Njoni kwangu, enyi nyote mnaonitamani,

Nanyi mjazwe mazao yangu.

20Ukumbusho wangu ni mtamu kuliko asali,

Na urithi wangu kupita sega la asali.

21Wanilao watakuwa wakali wana njaa,

Waninywao watakuwa wakali wana kiu,

22Mwenye kunitii hatatahayarika kamwe,

Wala wenye shughuli nami hawakosi.

Hekima na Sheria

23Mambo hayo yote ni Kitabu cha Agano la Mungu aliye juu;

24yaani, Torati ile ambayo Musa alituagiza ili iwe urithi kwa makusanyiko ya Yakobo.

25Ndiyo Torati ambayo hufanya hekima kuwa maridhawa kama Pishoni, na kama Tigri wakati wa matunda mapya;

26ambayo hufanya ufahamu kuwa umejaa kama Frati, na kama Yordani wakati wa mavuno;

27ambayo hufanya mafundisho kufurika kama mto Nile, na kama Gihoni wakati wa mavuno ya zabibu.

28Yule mtu wa kwanza hakuijua kamili, vivyo hivyo huyu wa mwisho hajamaliza kuichunguza.

29Kwa maana fikira zake zimetekwa baharini, na mashauri yake kutoka vilindini.

30Tazama, mimi nilitokea kama kijito kutoka kwa mto, na kama mfereji wa bustani.

31Nilisema, Nitatia maji bustani yangu, na kuyanywesha kwa wingi matuta yake; kumbe! Kijito kimekuwa mto, na mto umekuwa bahari.

32Hata sasa nitazidi kumulikia mafundisho kama alfajiri, nami nitayang'arisha hayo mpaka mbali.

33Nitakupua elimu kama unabii, na kuwaachia vizazi vitakavyokuja.

34Tazama, mimi sikujitahidi kwa ajili yangu mimi peke yangu, ila kwa ajili ya wote waitafutao hekima kwa bidii.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya