Wimbo ulio Bora 2

Wimbo ulio Bora 2

1Mimi ni ua la uwandani,[#2:1 kwa Kiebrania ni Sharoni.]

Ni fahirisi ya mabondeni.

2Kama fahirisi kati ya miiba,

Kadhalika mpenzi wangu kati ya binti.

3Kama mpera kati ya miti ya msituni,[#Mwa 3:6; Ufu 22:1]

Kadhalika mpendwa wangu kati ya vijana.

Niliketi kivulini mwake kwa furaha,

Na matunda yake niliyaonja kuwa matamu.

4Akanileta mpaka nyumba ya karamu,

Na bendera yake juu yangu ni mapenzi.

5Nishibisheni zabibu, niburudisheni kwa mapera,

Kwa maana nimezimia kwa mapenzi.

6Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,[#Wim 8:3]

Nao wa kulia unanikumbatia!

7Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,

Kwa paa na kwa ayala wa porini,

Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha,

Hata yatakapoona vema yenyewe.

8Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama, anakuja,[#Yn 10:4]

Akiruka milimani, akichachawa vilimani.

9Mpendwa wangu ni kama paa, au ayala.

Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu,

Achungulia dirishani, atazama kimiani.

10Mpendwa wangu alinena, akaniambia,

Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,

11Maana tazama, majira ya baridi yamepita,

Masika imekwisha, imekwenda zake;

12Maua yatokea katika nchi,

Wakati wa kuimba umefika,

Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu.

13Mtini wapevusha tini zake,

Na mizabibu inachanua,

Inatoa harufu yake nzuri;

Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako.

14Hua wangu, mafichoni mwa jabali,[#Wim 8:13]

Katika sitara za, magenge

Nitazame uso wako, nisikie sauti yako,

Maana sauti yako ni tamu na uso wako unapendeza.

15Tukamatie mbweha,[#Zab 80:13; Eze 13:4; Lk 13:32]

Wale mbweha wadogo,

Waiharibuo mizabibu,

Maana mizabibu yetu yachanua.

16Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake;[#Wim 6:3]

Hulisha kundi lake penye nyinyoro.

17Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie,[#Wim 4:6; Lk 1:78; Rum 13:12; 2 Pet 1:19; Wim 8:14]

Unigeukie, mpendwa wangu,

Nawe uwe kama paa, au ayala,

Juu ya milima ya Betheri.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya