The chat will start when you send the first message.
1Tazama, u mzuri, mpenzi wangu,[#Wim 1:15; 6:5]
U mzuri, macho yako ni kama ya hua,
Nyuma ya barakoa yako.
Nywele zako ni kama kundi la mbuzi,
Wakijilaza mbavuni pa mlima Gileadi.
2Meno yako ni kama kundi waliokatwa manyoya,[#Wim 6:6]
Wakipanda kutoka kuoshwa,
Ambao kila mmoja amezaa mapacha,
Wala hakuna aliyefiwa kati yao.
3Midomo yako ni kama uzi mwekundu,
Na kinywa chako ni kizuri;
Mashavu yako ni kama nusu kipande cha komamanga,
Nyuma ya barakoa yako.
4Shingo yako ni kama mnara wa Daudi,[#2 Sam 22:51; Wim 1:10; Neh 3:19]
Uliojengwa pa kuwekea silaha;
Ngao elfu zimetungikwa juu yake,
Zote ni ngao za mashujaa.
5Matiti yako mawili ni kama wanapaa wawili,[#Mit 5:19; Wim 1:13; Isa 66:10-12; 1 Pet 2:2]
Nyuma ya barakoa yako.
Ambao ni mapacha ya paa;
Wakilisha penye nyinyoro.
6Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie,
Nitakwenda kwenye mlima wa manemane,
Na kwenye kilima cha ubani.
7Mpenzi wangu, u mzuri kwa ujumla,[#Efe 5:27]
Wala ndani yako hamna kasoro.
8Bibi arusi, njoo pamoja nami toka Lebanoni,[#Kum 3:9]
Pamoja nami toka Lebanoni.
Shuka kutoka kilele cha Amana,
Kutoka vilele vya Seniri na Hermoni;
Kutoka mapangoni mwa simba,
Kutoka milimani mwa chui.
9Umenishangaza moyo, dada yangu,[#Isa 54:5; Yn 3:29; 2 Kor 11:2; Ufu 19:7,8]
Bibi arusi, umenishangaza moyo,
Kwa mtupo mmoja wa macho yako,
Kwa mkufu mmoja wa shingo yako.
10Jinsi pendo lako lilivyo nzuri, dada yangu,
Bibi arusi, ni nzuri kupita divai;
Na harufu ya marhamu yako
Yapita manukato ya kila namna.
11Bibi arusi, midomo yako yadondosha asali,[#Mit 24:13,14; Mwa 27:27; Hos 14:6,7]
Asali na maziwa viko chini ya ulimi wako;
Na harufu ya mavazi yako
Ni kama harufu ya Lebanoni.
12Bustani iliyofungwa ni dada yangu, bibi arusi,[#Isa 58:11; Hos 3:3]
Kijito kilichofungwa, chemchemi iliyotiwa mhuri.
13Machipuko yako ni bustani ya komamanga,
Yenye matunda mazuri, hina na nardo,
14Nardo na zafarani, mchai na mdalasini,
Na miti yote iletayo ubani,
Manemane na udi, na kolezi kuu zote.
15Wewe ndiwe chemchemi ya bustani yangu,[#Yn 4:10]
Kisima cha maji yaliyo hai,
Vijito vya Lebanoni viendavyo kasi.
16Amka, kaskazi; nawe uje, kusi;[#Gal 5:22; Wim 5:1]
Vumeni juu ya bustani yangu,
Manukato ya bustani yatokee.
Mpendwa wangu na aingie bustanini mwake,
Akayale matunda yake mazuri.