Wimbo ulio Bora 7

Wimbo ulio Bora 7

Maelezo ya wasifu

1Binti wa kimalkia, jinsi ulivyo mzuri[#Zab 45:13]

Hatua zako katika mitarawanda.

Mapaja yako ya mviringo ni kama johari,

Kazi ya mikono ya fundi stadi;

2Kitovu chako ni kama bakuli la mviringo,

Na isikose divai iliyochanganyika;

Tumbo lako ni mfano wa chungu ya ngano,

Iliyozungukwa na ugo wa nyinyoro;

3Matiti yako mawili ni kama wanapaa wawili,[#Wim 4:5]

Ambao ni mapacha ya paa;

4Shingo yako ni kama huo mnara wa pembe;

Macho yako kama viziwa vya Heshboni,

Karibu na mlango wa Beth-rabi;

Pua yako ni kama mnara wa Lebanoni,

Unaoelekea Dameski;

5Kichwa chako juu yako ni kama Karmeli,

Na nywele za kichwa chako kama urujuani,

Mfalme amenaswa na mashungi yake.

6Jinsi yalivyo mazuri, yalivyo matamu,

Mapenzi katikati ya anasa!

7Kimo chako kimefanana na mtende,

Na matiti yako na vichala.

8Nilisema, Nitapanda huo mtende,

Na kuyashika makuti yake.

Matiti yako na yawe kama vichala vya mzabibu,

Na harufu ya pumzi yako kama mapera;

9Na kinywa chako kama divai iliyo bora,

Kwa mpendwa wangu inashuka taratibu,

Ikitiririka midomoni mwao walalao.

10Mimi ni wake mpendwa wangu,[#Wim 2:16; Gal 2:20; Zab 45:11]

Na shauku yake ni juu yangu.

11Njoo, mpendwa wangu, twende mashambani,

Tufanye maskani katika vijiji.

12Twende mapema hadi mashamba ya mizabibu,[#Wim 6:11; 4:16; Zab 63:3-8; 73:25]

Tuone kama mzabibu umechanua,

Na maua yake yamefunuka;

Kama mikomamanga imetoa maua;

Huko nitakupa upendo wangu.

13Mitunguja hutoa harufu yake;[#Mwa 30:14; Wim 5:1; Mt 13:52; Yn 15:8]

Juu ya milango yetu yako matunda mazuri,

Mapya na ya kale, ya kila namna,

Niliyokuwekea, mpendwa wangu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya