The chat will start when you send the first message.
1Wakaendelea mpaka walipoukaribia Ninawi.
2Hapo Rafaeli alimwambia Tobia, Ndugu yangu, waijua hali uliyomwacha baba yako.
3Basi sasa tumtangulie mkeo, ili tukaitengeneze nyumba.
4Nawe uichukue mkononi mwako nyongo ya samaki. Basi wakashika njia mbele, na yule mbwa akafuatana nao.
5Naye Ana alikuwa amekaa kuyaelekeza macho yake njiani hali akimtazamia mwanawe.
6Akamwona mbwa akija mbio; akamwambia mumewe, Lo-o-o! Mwanao anakuja, na yule mtu aliyefuatana naye.
7Rafaeli akamwambia Tobia, Najua ya kuwa baba yako atafumbua macho yake.
8Basi umtie mara nyongo machoni; na imchomapo atajifikicha; na vyamba vyeupe vitaambuka; atakuona kwa macho.
9Lakini Ana alimkimbilia, akamwangukia mwanawe shingoni, akamwambia, Mwanangu! Nimekuona; tangu sasa ni radhi nife. Wakalia wote wawili.
10Tobiti naye akaondoka kwenda mlangoni, akajikwaa; lakini mwanawe akamkimbilia, akamshika baba yake;
11akamtia nyongo machoni, akasema, Jipe moyo, baba yangu.
12Yeye macho yake yalipoanza kuwasha aliyafikicha; navyo vyamba vyeupe vikaambuka katika pembe za macho yake,[#Mdo 9:18]
13akamwona mwanawe, akamwangukia shingoni.
14Akalia, akasema, Ee Mungu, umehimidiwa; na jina lako limehimidiwa milele; na watukuzwe malaika zako watakatifu wote.
15Kwa maana umenirudi, ukanihurumia; lo-o-o! Namwona mwanangu Tobia. Naye mwanawe aliingia ndani, huku anafurahi, akamwambia baba yake habari za yale mambo makuu yaliyomtukia huko Umedi.
16Ndipo Tobiti alipotoka mara kwenda kumlaki mkwewe penye lango la Ninawi, akifurahi na kumhimidi Mungu; na wale waliomwona akienda wakastaajabu, kwa sababu amepewa kuona tena.
17Naye Tobiti akashukuru mbele yao, kwa sababu Mungu amemrehemu, na alipomkaribia mkwewe Sara, alimbariki, akasema, Binti yangu, karibu kwetu. Amehimidiwa Mungu aliyekuleta kwetu, na baba yako na mama yako wamebarikiwa. Ikawa furaha kuu kwa ndugu zake zote waliokuwako Ninawi.
18Akaja Akiakaro, pamoja na Nasba mwana wa nduguye; akafanywa karamu ya arusi yake Tobia siku saba kwa furaha kuu.