The chat will start when you send the first message.
1Basi Tobia akajibu, akamwambia, Baba nitatenda yote uliyoniagiza;
2lakini niwezeje kuipokea ile fedha, nami simfahamu yule?
3Basi alimpa ile hati; akamwambia, Kajitafutie mtu atakayefuatana nawe, nami nitampa mshahara wake nikiwa bado hai; kisha uende ukaipokee ile fedha.
4Ikawa alipokwenda kutafuta mtu, alikutana na Rafaeli, naye yu malaika aliyetokea katika umbo linaloonekana.[#Ebr 13:2; #5:4 Katika vitabu vya kwanza vya Biblia ‘Malaika wa Bwana’ au ‘Malaika wa Mungu’ alikuwa Mungu mwenyewe.]
5Lakini yeye hana habari, akamwambia, Je! Waweza kufuatana nami mpaka Rage, mji wa Umedi; na mahali wapajua sawasawa?
6Malaika akamwambia, Mimi nitakwenda nawe, nami naijua sana njia; hata nimekaribishwa kwake ndugu yetu Gabaeli.
7Basi Tobia akamwambia, Haya! Ningoje kwanza hata nikamwambie baba yangu.
8Akamwambia, Nenda basi, usikawie. Basi akaingia, akamwambia baba yake, Tazama, nimemwona mtu atakayekwenda pamoja nami. Akamjibu, Kamwite aje kwangu, nimfahamu yu wa kabila gani; na kama yu mtu mwaminifu afaaye kwenda nawe.
9Akamwita, naye akaja.
10Wakasalimiana.
11Tobiti akamwambia, Ndugu, unijulishe kabila lako na jamaa yako.
12Akamwambia, Je! Watafuta kabila na jamaa, au mtu wa mshahara kwenda na mwanao? Tobiti akamwambia, Ndugu, nina haja kujua jamaa yako na jina lako.
13Basi akasema, Mimi ni Azaria, mwana wake Anania mkuu, ni wa ndugu zako.
14Tobiti akamwambia, Ee ndugu, karibu; usinikasirikie kwa sababu nilitafuta habari za kabila lako na jamaa yako; maana ndiwe uliye ndugu yangu wa ukoo mwema mzuri. Kweli niliwafahamu Anania na Yonathani, wana wa Shemaya mkuu, tulipokuwa tukienda wote Yerusalemu ili kuabudu. Tulikuwa tukitoa wazalia wa kwanza, na zaka za mazao yetu; wala hao hawakupotoka kwa kulifuatisha kosa la ndugu zetu. Ndugu yangu, wewe u mtu wa ukoo mstahifu.
15Lakini sasa uniambie, nikupe mshahara gani? Je! Shilingi kutwa na riziki yako, kama apatavyo mwanangu?
16Tena, mkirudi salama, nitatoa faida zaidi ya mshahara wako. Wakapatana.[#Mwa 24:7,40]
17Akamwambia Tobia, Kajiweke tayari kwa safari; naye Mungu akujalieni safari njema. Naye mwanawe alipokwisha kuyaweka tayari mahitaji yake ya safari, baba yake akamwambia, Nenda na mtu huyu; na Mungu akaaye mbinguni ataifanikisha safari yenu; na malaika wake afuatane nanyi. Hivyo wakaondoka wote wawili, na mbwa wa yule kijana akafuatana nao.
18Bali Ana, mama yake, akalia; akamwambia Tobiti, Mbona umemsafirisha mtoto wetu? Siye fimbo yetu ya mkononi, kwa kuingia na kutoka mbele yetu?
19Usifanye choyo kutaka kuongeza fedha juu ya fedha; bali na iwe kama kifusi kuliko mtoto wetu.
20Kwa maana kadiri BWANA alivyotupa kuishi, ndivyo itutoshavyo.
21Tobiti akamjibu, Mwenzangu, usijisumbue; yeye atarudi salama, na macho yako yatamwona.
22Kwa maana malaika mwema atafuatana naye na safari yake itafanikiwa, naye atarudi salama salimini.