1 Wakorintho 4

1 Wakorintho 4

Mitume wa Kristo Yesu

1Tuchukulieni sisi kuwa ni watumishi wa Kristo, ambao Mungu ametuamini tufanye kazi ya kuwaambia wengine siri zake za kweli.

2Wale walioaminiwa kwa kazi muhimu kama hii imewapasa kuonesha ya kuwa wao ni waaminifu.

3Lakini siichukulii hukumu yenu kuhusu hili kuwa kitu. Hata hukumu yoyote katika mahakama ya kibinadamu isingekuwa na maana yoyote. Sijihukumu hata mimi mwenyewe.

4Sikumbuki kosa lolote nililofanya, lakini hiyo hainifanyi mimi kujihesabia haki. Bwana pekee ndiye anayepaswa kunihukumu ikiwa nimefanya vyema au la.

5Hivyo, msimhukumu mtu yeyote sasa. Hukumu itakuwa wakati Bwana atakaporudi. Ataangaza mwanga kwa kila kitu kilichofichwa gizani. Ataziweka wazi nia za siri za mioyo yetu. Ndipo sifa ambayo kila mtu anapaswa kuipata itatoka kwa Mungu.

6Ndugu zangu, nimemtumia Apolo na mimi mwenyewe kama mfano kwa ajili yenu. Nimefanya hivi ili mjifunze kutoka kwetu maana ya maneno yanayosema, “Uwe mwangalifu kufuata kilichoandikwa.”[#4:6 Kwa maana ya kawaida, “Msifanye zaidi ya kile kilichoandikwa”. Hii ina maana ya Maandiko ama usemi maarufu, mfumo ama kanuni kwamba walimu walitumia watoto kuandika alfabeti. Paulo anawatia moyo Wakorintho wafuate mfano huo.]

7Kwa nini mnajisifu? Mlipewa kila kitu mlicho nacho. Sasa, ikiwa mlipewa kila kitu mlicho nacho, kwa nini mnajisifu kana kwamba mlipata vitu vyote kwa nguvu zenu wenyewe?

8Mnadhani kwamba tayari mna kila kitu mnachohitaji. Mnadhani kwamba mmekwisha tajirika. Laiti mngekwisha fanywa wafalme, kwa sababu tungekuwa wafalme pamoja nanyi.

9Lakini inaonekana kana kwamba Mungu amenipa mimi na mitume wengine mahali pa mwisho. Sisi ni kama wafungwa waliohukumiwa kufa, waliosimamishwa katika gwaride ili ulimwengu wote uwaone, si watu tu bali hata malaika pia.

10Tu wapumbavu kwa kuwa sisi ni wa Kristo, lakini mnadhani kuwa ninyi ni wenye hekima katika Kristo. Sisi ni dhaifu, lakini mnadhani kuwa mna nguvu. Watu wanawaheshimu ninyi, na hawatuheshimu sisi.

11Hata sasa hatuna vyakula vya kutosha kula au kunywa, na hatuna nguo za kutosha. Mara kwa mara tunapigwa na hatuna makazi.

12Tunafanya kazi sana kwa mikono yetu ili tupate chakula. Watu wanapotutukana, tunamwomba Mungu awabariki. Watu wanapotutendea vibaya, tunavumilia.

13Watu wanaposema mabaya juu yetu, tunawajibu kwa upole. Lakini watu wanaendelea kutuona kama takataka.

14Siwaambii haya ili kuwatahayarisha, lakini ninaandika haya ili kuwaonya kama watoto wangu mwenyewe ninaowapenda.

15Mnaweza kuwa na walimu elfu kumi katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Kupitia Habari Njema mimi nilifanyika baba kwenu katika Kristo Yesu.

16Ndiyo sababu ninawahimiza mfuate mfano wangu.

17Ndiyo sababu ninamtuma Timotheo kwenu. Ni mwanangu katika Bwana. Ninampenda na ni mwaminifu. Atawasaidia ili mkumbuke namna ninavyoishi kama mfuasi wa Kristo Yesu, kama ninavyofundisha katika kila kanisa kila mahali ninakokuwa.

18Baadhi yenu mnajivuna, mkidhani kuwa sitakuja kuwatembelea tena.

19Lakini nitakuja kwenu hivi karibuni ikiwa Bwana atanijalia. Ndipo nitajua ikiwa hawa wanaojivuna wana nguvu za kutenda jambo lolote zaidi ya kuzungumza.

20Mungu huonesha kuwa anatawala katika maisha kwa yale wanayoweza kufanya na si kwa maneno yao.

21Je! nitakapokuja kwenu, nije nikiwa na adhabu au nije kwa upendo na upole?

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International