1 Wakorintho 5

1 Wakorintho 5

Msiwaruhusu Watu Wenu Waishi Katika Dhambi

1Sitaki kuyaamini yale ninayosikia, ya kwamba kuna uzinzi katikati yenu. Na ni aina mbaya ya uzinzi ambayo hata wasiomwamini Mungu wetu hawauruhusu. Watu wanasema kuwa huko kwenu kuna mtu anayetenda dhambi ya zinaa na mke wa baba yake.

2Na mna kiburi! Mngepaswa kuwa na huzuni badala yake. Na mtu aliyetenda dhambi hiyo ilipaswa kuwa amefukuzwa kutoka katika kundi lenu.

3Siwezi kuwa hapo pamoja nanyi ana kwa ana, lakini niko pamoja nanyi katika roho. Na nimekwisha mhukumu mtu aliyetenda hii kama ambavyo ningemhukumu ikiwa ningekuwa hapo.

4Nanyi pia mnapaswa kufanya vivyo hivyo. Kusanyikeni pamoja katika jina la Bwana wetu Yesu. Nitakuwa pamoja nanyi katika roho, na nguvu ya Bwana Yesu itakuwa pamoja nanyi.

5Mtoeni mtu huyu kwa Shetani ili tabia yake ya kujisifu iangamizwe lakini mtu mwenyewe na kanisa, lilojazwa Roho, liweze kuokolewa siku Bwana atakaporudi.[#5:5 Kwa maana ya kawaida, “Mwili wa dhambi”, ama “damu na nyama”.]

6Kujisifu kwenu si kuzuri. Mnajua msemo unaosema, “Chachu kidogo huchahua donge zima.”

7Ondoeni chachu ya zamani ili muwe donge jipya. Ninyi kwa hakika ni mkate usio na chachu, mkate wa Pasaka, Ndiyo, Kristo aliye Mwanakondoo wetu wa Pasaka amekwisha usawa.[#5:7 Mkate maalum usio na chachu (chachu) ambao Wayahudi walikula katika mlo wa Pasaka. Paulo anamaanisha kuwa waamini hawana dhambi, kama ambavyo mkate wa Pasaka haukuwa na chachu.; #5:7 Yesu alikuwa sadaka kwa ajili ya watu wake, kama mwanakondoo aliyechinjwa kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka ya Kiyahudi.]

8Hivyo na tuule mlo wetu wa Pasaka, lakini si pamoja na mkate wenye chachu ya zamani, yaani dhambi na matendo mabaya. Lakini tule mkate usio na chachu. Huu ni mkate wenye ukweli na chachu njema.

9Katika barua yangu niliwaandikia kuwa msishirikiane na wazinzi.

10Lakini sikuwa na maana ya watu wa ulimwengu huu. La sivyo ingewalazimu kuhama katika ulimwengu huu ili mweze kujitenga na wazinzi au walio walafi na waongo, au wale wanaoabudu sanamu.

11Nilikuwa na maana kuwa msishirikiane na mtu yeyote yule anayedai kuwa anaamini lakini anaendelea kuishi katika dhambi. Usimkaribishe nyumbani kwa chakula kaka ama dada aliye mzinzi, mlafi, anayeabudu sanamu, mtukanaji, mlevi au mwongo.[#5:11 Kulaghai watu ili kuwaibia.]

12-13Si kazi yangu kuwahukumu wasio sehemu ya kundi la waamini. Mungu atawahukumu, lakini ni lazima mwahukumu wale walio katika kundi lenu. Maandiko yanasema, “Mwondoe mwovu katika kundi lako.”[#Kum 22:21,24]

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International