The chat will start when you send the first message.
1Kutoka kwa Yakobo mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo.
Kwa makabila Kumi na Mawili ya watu wa Mungu yaliyotawanyika kote ulimwenguni: Salamu!
2Kaka na dada zangu, jueni kuwa mtakutana na adha za kila aina. Lakini hilo liwape ninyi sababu ya kuwa na furaha zaidi.
3Kwa sababu mnajua kuwa imani yenu inapojaribiwa ndipo mnapojifunza kuwa wavumilivu.
4Na uvumilivu unapaswa kukamilisha kazi yake, ili kwamba muwe watu waliokomaa na wakamilifu msiopungukiwa na kitu cho chote.
5Hivyo kama mmoja wenu atapungukiwa na hekima, anapaswa kumwomba Mungu anayewapa watu wote kwa ukarimu, naye atampa hekima.
6Lakini anapaswa kuwa na imani anapoomba pasipo mashaka yoyote, kwani yule aliye na mashaka ni kama wimbi la baharini, linalosukumwa na upepo na kusukwa sukwa.
7Mtu wa jinsi hiyo asidhani kuwa anaweza kupokea cho chote kutoka kwa Bwana;
8yeye ni mwenye mashaka na hufikiria mambo mawili tofauti kwa wakati mmoja.
9Ndugu aliye maskini na awe na furaha sana kwamba Mungu amemchukulia kuwa mtu wa maana sana.
10Na waaminio walio matajiri wawe na furaha sana tu pale Mungu anapowashusha chini. Kwani utajiri wao hautawazuia kufa kama maua ya porini.
11Jua linapochomoza na kuwa kali zaidi, joto lake hukausha mimea na maua huanguka chini na kupukutika na kupoteza urembo wake. Kwa jinsi hiyo hiyo, mtu tajiri atafifia katika shughuli zake.
12Amebarikiwa mtu yule anayestahimili majaribu, maana anapofaulu mitihani atapokea taji yenye uzima ambayo Mungu amewaahidi wale wanaompenda.
13Yeyote anayejaribiwa hapaswi kusema, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu maovu hayamjaribu Mungu na hamjaribu mtu yeyote.
14Bali kila mmoja anajaribiwa na tamaa zake mwenyewe, anapovutwa na kunaswa.
15Kisha tamaa inapotunga mimba inazaa dhambi, na dhambi ikikomaa kabisa inazaa kifo.
16Kaka zangu na dada zangu wapendwa msikubali kudanganywa,
17Kila karama njema na kila tuzo kamilifu hutoka juu; hushuka chini kutoka kwa Baba aliyeumba nuru zote zilizoko mawinguni ambamo kwake yeye hakuna mabadiliko kama vile vivuli vinavyosababishwa na mzunguko wa sayari.
18Kwa uamuzi wake mwenyewe Mungu alituzaa sisi na kuwa watoto wake kwa njia ya ujumbe wa kweli ili tuwe mazao ya kwanza yenye heshima ya pekee miongoni mwa vyote alivyoviumba.[#1:18 Kwa Waisraeli “mazao ya kwanza” yalikuwa sehemu ya kwanza ya mazao ambayo walileta kwa Kuhani kwa ajili ya kumtolea Mungu. Paulo amelitumia neno hili kwa kanisa. Hapa neno hili limetumika kwa maana ya heshima maalumu ambayo waaminio wanayo mbele ya Mungu tofauti na viumbe vyote. Hawa wanategemea uumbaji mpya na ukombozi ambao wanadamu watakutana nao katika mbingu mpya.]
19Kumbukeni hili ndugu zangu wapendwa: Kila mtu awe mwepesi wa kusikia lakini awe mzito wa kusema, na mzito kukasirika,
20kwa sababu hasira ya mwanadamu haitoi haki inayohitajiwa na Mungu toka kwetu.
21Hivyo acheni matendo yote machafu na kila uovu uliokaa karibu yenu, na mpokee kwa unyenyekevu mafundisho yaliyopandwa ndani ya mioyo yenu. Neno hilo, lina uwezo wa kuleta wokovu wa roho zenu.
22Usisikilize tu kile ambacho mafundisho ya Mungu yanakisema; bali fanya yale inayosema! Ikiwa utasikiliza tu, utajidanganya mwenyewe.
23Kwani kama mtu atasikiliza mafundisho ya Mungu, lakini asitende yanayosemwa, yuko kama mtu anayeutazama uso wake kwenye kioo.
24Anajiangalia mwenyewe kwa haraka na anapoondoka tu husahau anavyoonekana.
25Lakini anayetazama kwa makini katika sheria kamilifu ya Mungu, inayowaletea watu uhuru, na akaendelea kufanya hivyo asiwe msikilizaji anayesahau, bali huyatunza mafundisho katika matendo, mtu huyo atakuwa na baraka katika kila analofanya.
26Kama kuna anayedhani kuwa ni mshika dini, lakini bado hauzuii ulimi wake anajidanganya mwenyewe. Dini yake mtu huyu haina manufaa.
27Dini safi na isiyo na lawama mbele za Mungu Baba, inahusisha haya: kuwatunza yatima na wajane katika mazingira mgumu na kujilinda asichafuliwe na ulimwengu.