The chat will start when you send the first message.
1Kaka zangu na dada zangu, ninyi ni wenye imani katika Bwana wetu mtukufu Yesu Kristo. Kwa hiyo msiwachukulie baadhi ya watu kuwa wa maana zaidi kuliko wengine.
2Tuchukulie mtu mmoja anakuja katika mkutano wenu akiwa amevaa pete ya dhahabu ama akiwa amevaa mavazi ya thamani, na mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa na machafu naye akaja ndani.
3Na tuchukulie kuwa mnaonyesha kumjali zaidi yule mtu aliyevaa mavazi mazuri na kusema, “Wewe keti hapa katika kiti hiki kizuri.” Lakini unamwambia yule mtu maskini, “Wewe simama pale,” au, “Keti chini karibu na miguu yetu.”
4Je! hiyo haioneshi kwamba mnafikiri miongoni mwenu kuwa baadhi ya watu ni bora kuliko wengine? Mmesimama kama mahakimu wenye maamuzi mabaya?
5Sikilizeni kaka na dada zangu wapendwa! Mungu aliwachagua wale walio maskini machoni pa watu kuwa matajiri katika imani. Aliwachagua kuwa warithi wa Ufalme, ambao Mungu aliwaahidi wale wanaompenda?
6Lakini ninyi mmewadhalilisha walio maskini! Na kwa nini mnawapa heshima kubwa watu walio matajiri? Hawa ndiyo wale ambao daima wanajaribu kuyadhibiti maisha yenu. Si ndiyo hao wanaowapeleka ninyi mahakamani?
7Je! si ndiyo hao hao wanaolitukana Jina zuri la Bwana wenu?[#2:7 Au “ambaye ninyi ni watu wake”.]
8Kama kweli mnaitunza sheria ya ufalme inayopatikana katika Maandiko, “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe,” mtakuwa mnafanya vizuri.[#2:8 Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.; #Law 19:18]
9Lakini kama mtakuwa mnaonyesha upendeleo, mtakuwa mnafanya dhambi na mtahukumiwa kuwa na hatia kama wavunja sheria.
10Ninasema hivi kwa sababu yeyote anayeitunza Sheria yote, lakini akaikosea hata mmoja tu atakuwa na hatia ya kuihalifu Sheria yote.
11Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” pia ndiye aliyesema, “Usiue.” Hivyo, kama hutazini lakini ukaua utakuwa umevunja Sheria yote ya Mungu.[#Kut 20:14; Kum 5:18; #Kut 20:13; Kum 5:17]
12Mseme na kutenda kama watu watakaokuja kuhukumiwa kwa sheria inayoleta uhuru.
13Kwa kuwa hukumu ya Mungu haitakuwa na huruma kwake yeye ambaye hakuwa na rehema. Lakini rehema huishinda hukumu!
14Ndugu zangu, ikiwa mtu atasema kuwa anayo imani lakini hafanyi kitu, imani hiyo haina manufaa yoyote. Imani ya jinsi hiyo haiwezi kumwokoa mtu yeyote.
15Kama ndugu au dada anahitaji mavazi na anapungukiwa chakula cha kila siku,
16na ukawaambia, “Mungu awe nanyi! Mkahifadhiwe mahala pa joto na mle vizuri!” Hiyo ina manufaa gani kwao? Usipowapa vitu wanavyovihitaji, maneno yako yanakosa maana!
17Kwa jinsi hiyo hiyo, imani isipokuwa na matendo itakuwa imekufa.
18Lakini mtu anaweza kuleta hoja kusema, “Watu wengine wanayo imani, na wengine wanayo matendo mema.” Jibu langu litakuwa, huwezi kunionyesha imani yako pasipo kufanya tendo lolote. Lakini mimi nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.
19Je! mnaamini kwamba kuna Mungu mmoja tu? Vema! Hata mapepo yanaamini na kutetemeka kwa hofu.
20Wewe mjinga! Je! unahitaji uthibitisho kwamba imani bila matendo haina manufaa?
21Je! si baba yetu Abrahamu alihesabiwa haki na Mungu kwa matendo yake alipomtoa sadaka mwanae Isaka juu ya madhabahu?
22Kwa hakika unaweza kuiona imani hiyo ilifanya kazi pamoja na matendo yake. Kwa hiyo imani yake ilikamilishwa na matendo yake.
23Ndipo yakatimizwa yale yaliyo kwenye Maandiko kuwa, “Abrahamu alimwamini Mungu, na kwa imani hiyo akafanywa kuwa mwenye haki kwa Mungu,” na kwa sababu hiyo akaitwa “Rafiki wa Mungu”.[#2:23 Ama alithibitishwa kuwa mwenye haki kama vile tafsiri zingine za walimu wa Biblia wangependa kutumia.; #Mwa 15:6; #2 Nya 20:7; Isa 41:8]
24Mnamwona mtu huyo amefanywa kuwa mwenye haki kwa Mungu kwa matendo yake wala siyo kwa imani peke yake.
25Je! Rahabu yule kahaba si alifanywa kuwa mwenye haki na Mungu kwa matendo aliyofanya, alipowasaidia wale waliokuwa wakipeleleza nchi kwa niaba ya watu wa Mungu. Aliwakaribisha nyumbani mwake na kuwawezesha kutoroka kwa njia nyingine.[#2:25 Simulizi juu ya Rahabu inapatikana katika Yos 2:1-21.]
26Hivyo, kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo, imani imekufa ikiwa haina matendo.