The chat will start when you send the first message.
1Yesu akasema, “Msisumbuke. Mwaminini Mungu, na mniamini na mimi.
2Kuna vyumba vya kutosha katika nyumba ya Baba yangu. Nisingewaambia hivi ikiwa isingelikuwa kweli. Ninaenda huko kuandaa mahali kwa ajili yenu.
3Nitakapomaliza kuandaa, nitarudi. Kisha nitawachukua ili muwe pamoja nami mahali niliko.
4Mnaijua njia iendayo kule ninakokwenda.”
5Thomaso akasema, “Bwana, hatujui unakokwenda, sasa tutaijuaje njia?”
6Yesu akajibu, “Mimi ndiye njia, kweli, na uzima. Njia pekee ya kwenda kwa Baba ni kupitia kwangu.
7Kwa kuwa sasa ninyi nyote mmenijua, mtamjua Baba yangu pia. Kwa kweli, sasa mnamjua Baba na mmekwisha kumwona.”
8Filipo akamwambia, “Bwana, utuonyeshe Baba. Hilo tu ndilo tunalohitaji.”
9Yesu akajibu, “Nimekuwa pamoja nanyi kwa kipindi kirefu. Hivyo wewe, Filipo unapaswa kunijua. Yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba pia. Hivyo kwa nini unasema, ‘Utuonyeshe Baba’?
10Hamwamini kuwa mimi nimo ndani ya Baba na Baba naye yumo ndani yangu? Mambo niliyowaambia hayatoki kwangu. Baba anakaa ndani yangu, naye anafanya kazi yake mwenyewe.
11Mniamini ninaposema kwamba nimo ndani ya Baba na Baba yumo ndani yangu. Vinginevyo muamini kwa sababu ya miujiza niliyoifanya.
12Hakika nawaambia, yeyote anayeniamini atafanya mambo kama yale niliyoyafanya. Naye atafanya mambo makubwa zaidi ya yale niliyofanya, kwa sababu mimi naenda kwa Baba.
13Na kama mtaomba jambo lo lote kwa jina langu, nitawafanyia. Kisha utukufu wa Baba utadhihirishwa kupitia kwa Mwana wake.
14Ikiwa mtaniomba chochote kwa jina langu, mimi nitakifanya.
15Ikiwa mnanipenda, mtafanya ninayowaagiza.
16Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine atakayekuwa nanyi siku zote.[#14:16 Au “Mfariji”, Roho Mtakatifu (tazama katika Orodha ya Maneno). Pia katika 14:26; 15:26; 16:7,8.]
17Huyo Msaidizi ni Roho wa Kweli ambaye watu wa ulimwengu hawawezi kumpokea, kwa sababu hawamwoni wala hawamjui. Lakini ninyi mnamjua kwa kuwa anakaa pamoja nanyi, na atakuwa ndani yenu.
18Mimi sitawaacha peke yenu kama watu wasiokuwa na wazazi. Bali nitakuja tena kwenu.
19Katika kipindi kifupi watu wa ulimwengu hawataniona tena. Lakini ninyi mtaniona. Mtaishi kwa sababu mimi ninaishi.
20Katika siku hiyo mtaelewa kuwa mimi nimo ndani ya Baba. Kadhalika mtajua pia kuwa ninyi mmo ndani yangu nami nimo ndani yenu.
21Wale wanaonipenda kweli ni wale ambao si tu kwamba wanazijua amri zangu bali pia wanazitii. Baba yangu atawapenda watu wa jinsi hiyo, nami pia nitawapenda. Nami nitajitambulisha kwao.”
22Kisha Yuda (siyo Yuda Iskariote) akasema, “Bwana, utawezaje kujitambulisha kwetu, lakini si kwa ulimwengu?”
23Yesu akajibu, “Wale wote wanipendao watayafuata mafundisho yangu. Naye Baba yangu atawapenda. Kisha Baba yangu na mimi tutakuja kwao na kukaa pamoja nao.
24Lakini yeyote asiyenipenda hafuati mafundisho yangu. Mafundisho haya mnayosikia kwa hakika siyo yangu. Ni kutoka kwa Baba yangu aliyenituma.
25Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi.
26Lakini yule Msaidizi atawafundisha kila kitu na kuwafanya mkumbuke kila nilichowaambia. Huyu Msaidizi ni Roho Mtakatifu ambaye Baba atamtuma kwa jina langu.[#14:26 Pia anaitwa Roho wa Mungu, Roho wa Kristo, na Mfariji. Katika muungano na Mungu na Kristo, hufanya kazi za Mungu miongoni mwa watu ulimwenguni.]
27Nawaachia amani. Ninawapa amani yangu mwenyewe. Ninawapa amani kwa namna tofauti kabisa na jinsi ulimwengu unavyofanya. Hivyo msihangaike. Msiogope.
28Mlinisikia nikiwaambia, ‘Naondoka, lakini nitakuja tena kwenu.’ Mngenipenda, mngefurahi kuwa naenda kwa Baba, kwa sababu Baba ni mkuu kuliko mimi.
29Nawaambia haya hivi sasa, kabla hayajatokea. Kisha yatakapotokea, mtaamini.
30Sitaendelea kuongea nanyi kwa muda mrefu zaidi. Mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Hata hivyo hana nguvu juu yangu.[#14:30 Huu ni Shetani. Tazama katika Orodha ya Maneno.]
31Lakini ni lazima ulimwengu utambue kuwa ninampenda Baba. Hivyo ninafanya yale Baba aliyoniambia.
Njooni sasa, twendeni.”