Isaya 65

Isaya 65

Mungu huwaadhibu waasi

1Mwenyezi-Mungu asema;[#65:1 Taz Rom 10:20]

“Nilikuwa tayari kujionesha

kwao wasiouliza habari zangu.

Nilikuwa tayari kuwapokea

wale wasionitafuta.

Nililiambia taifa ambalo halikuomba kwa jina langu:

‘Nipo hapa! Nipo hapa!’

2Mchana kutwa niliwanyoshea mikono watu waasi,[#65:2 Taz Rom 10:21]

watu ambao hufuata njia zisizo sawa,

watu ambao hufuata fikira zao wenyewe.

3Ni watu ambao daima hunichokoza waziwazi;

hutambikia miungu yao katika bustani,

na kuifukizia ubani juu ya matofali.

4Huketi makaburini na kukaa mafichoni usiku.

Hula nyama ya nguruwe na mchuzi wa wanyama haramu.

5Huwaambia wale wanaokutana nao:

‘Kaeni mbali nami;

msinikaribie kwani mimi ni mtakatifu!’

Watu hao wananikasirisha mno,

hasira yangu ni kama moto usiozimika.

6“Jueni kuwa nimelitia jambo hilo moyoni,

sitanyamaza bali nitawafanya walipe;

nitawafanya walipe kwa wingi.

7Mimi Mwenyezi-Mungu, nitawalipiza maovu yao

wayalipie na maovu ya wazee wao.

Wao waliifukizia ubani miungu yao milimani,

wakanitukana mimi huko vilimani.

Nitawafanya walipe kwa wingi,

watayalipia matendo yao ya awali.”

8Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Mtu akikuta kishada cha zabibu nzuri,

watu husema: ‘Tusikiharibu; kina baraka.’

Ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu;

sitawaangamiza wote.

9Nitawajalia watu wa Yakobo,

na Yuda nitamjalia warithi wa milima yangu;

watumishi wangu watakaa huko.

10Nchi tambarare ya Sharoni itakuwa malisho,[#65:10 Taz Yos 7:24-26]

bonde la Akori litakuwa mapumziko ya mifugo

kwa ajili ya watu wangu walionitafuta.

11“Lakini nitafanya nini na nyinyi

mnaoniacha mimi Mwenyezi-Mungu,

msioujali Siyoni, mlima wangu mtakatifu,

nyinyi mnaoabudu mungu ‘Gadi’,

na kumtolea tambiko ya divai mungu ‘Meni’?

12Nimewapangia kifo kwa upanga,

nyote mtaangukia machinjoni!

Maana, nilipowaita, hamkuniitikia;

niliponena, hamkunisikiliza.

Mlitenda yaliyo maovu mbele yangu,

mkachagua yale nisiyoyapenda.

13Basi, mimi Mwenyezi-Mungu nasema,

watumishi wangu watakula,

lakini nyinyi mtaona njaa;

watumishi wangu watakunywa,

lakini nyinyi mtaona kiu;

watumishi wangu watafurahi,

lakini nyinyi mtafedheheka.

14Watumishi wangu wataimba kwa furaha moyoni,

lakini nyinyi mtalia kwa uchungu moyoni

na kupiga kelele kwa uchungu mkubwa rohoni.

15Wale niliowachagua nitawapa jina jipya.

Lakini nyinyi jina lenu watalitumia kulaania;

‘Watasema: Bwana Mungu awaue kama hao.’

16Basi, mwenye kujitakia baraka nchini,

atajitakia baraka kwa Mungu wa kweli.

Mwenye kuapa katika nchi hii,

ataapa kwa Mungu wa kweli.

Maana taabu za zamani zimepita

zimetoweka kabisa mbele yangu.

Ulimwengu mpya

17“Sasa, naumba mbingu mpya na dunia mpya.[#65:17 Taz Isa 66:22; 2Pet 3:13; Ufu 21:1]

mambo ya zamani hayatakumbukwa tena.

18Furahini, mkashangilie milele,

kwa ajili ya vitu hivi ninavyoumba.

Yerusalemu nitaufanya mji wa shangwe,

na watu wake watu wenye furaha.

19Nami nitaufurahia mji wa Yerusalemu,[#65:19 Taz Ufu 21:4]

nitawafurahia watu wangu.

Sauti ya kilio haitasikika tena,

kilio cha taabu hakitakuwako.

20Hakutakuwa tena na vifo vya watoto wachanga,

wazee nao hawatakufa kabla ya wakati wao.

Akifa mtu wa miaka 100 amekufa akiwa kijana;

na akifa kabla ya miaka 100 ni balaa.

21Watu watajenga nyumba na kuishi humo;

watalima mizabibu na kula matunda yake.

22Hawatajenga nyumba zikaliwe na watu wengine,

wala kulima chakula kiliwe na watu wengine.

Maana watu wangu niliowachagua

wataishi maisha marefu kama miti;

wateule wangu watafurahia matunda ya jasho lao.

23Kazi zao hazitakuwa bure,

wala hawatazaa watoto wa kupata maafa;

maana watakuwa waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu,

wamebarikiwa wao pamoja na wazawa wao.

24Hata kabla hawajaniita, mimi nitawaitikia;

kabla hawajamaliza kusema, nitakuwa nimewajibu.

25Mbwamwitu na kondoo watakula pamoja,[#65:25 Taz Isa 11:6-9]

simba watakula nyasi kama ng'ombe,

nao nyoka chakula chao kitakuwa vumbi.

Katika mlima wangu wote mtakatifu,

hakuna atakayeumiza au kuharibu kitu.

Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania