Zaburi 136

Zaburi 136

Wimbo wa shukrani

1Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema;[#Taz Zab 100:5; 106:1; 107:1; 118:1]

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

2Mshukuruni Mungu wa miungu;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

3Mshukuruni Bwana wa mabwana;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

4Ndiye peke yake atendaye makuu ya ajabu;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

5Ndiye aliyeziumba mbingu kwa hekima;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

6Ndiye aliyeitengeneza nchi juu ya vilindi vya maji;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

7Ndiye aliyeumba jua, mwezi na nyota;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

8Jua liutawale mchana;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

9Mwezi na nyota vitawale usiku;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

10Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza wa Misri;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

11Akawaondoa watu wa Israeli kutoka huko;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

12Kwa mkono wake wenye nguvu na enzi;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

13Ndiye aliyeigawa Bahari ya Shamu sehemu mbili;

kwa maana fadhili zake zadumu milele,

14akawapitisha watu wa Israeli humo;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

15Lakini akawazamisha humo Farao na jeshi lake;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

16Ndiye aliyewaongoza watu wake jangwani;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

17Ndiye aliyewapiga wafalme wenye nguvu;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

18Akawaua wafalme maarufu;

kwa maana fadhili zake zadumu milele;

19akamuua Sihoni, mfalme wa Waamori,

kwa maana fadhili zake zadumu milele;

20na Ogu, mfalme wa Bashani;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

21Akachukua nchi zao akawapa watu wake;

kwa maana fadhili zake zadumu milele;

22ziwe riziki ya Israeli, mtumishi wake;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

23Ndiye aliyetukumbuka wakati wa unyonge wetu;

kwa maana fadhili zake zadumu milele;

24akatuokoa kutoka maadui zetu;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

25Ndiye akipaye kila kiumbe chenye uhai chakula;

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

26Mshukuruni Mungu wa mbinguni;

kwa maana fadhili zake zadumu milele!

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania