The chat will start when you send the first message.
1Dunia na vyote vilivyomo ni vyake Mwenyezi-Mungu;[#Taz 1Kor 10:26]
ulimwengu na wote waishio humo ni mali yake.
2Maana yeye aliweka misingi ya dunia juu ya bahari;
aliisimika imara juu ya mito ya maji.
3Nani atakayepanda mlima wa Mwenyezi-Mungu?
Nani atakayekaa katika hekalu lake takatifu?
4Ni mtu wa matendo mema na moyo safi,[#Taz Mat 5:8]
asiyeuelekeza moyo wake katika upuuzi,
wala kuapa kwa uongo.
5Mtu huyo atapokea baraka kwa Mwenyezi-Mungu,
na haki yake kwa Mungu mwokozi wake.
6Ndio hali ya kizazi cha watu wamtafutao yeye;
naam, watu wamtafutao Mungu wa Yakobo.
7Fungukeni enyi milango;
fungukeni enyi milango ya kale,
ili Mfalme mtukufu aingie.
8Ni nani huyo Mfalme mtukufu?
Ni Mwenyezi-Mungu, mwenye nguvu na uwezo;
Mwenyezi-Mungu, mwenye uwezo vitani.
9Fungukeni enyi malango,
fungukeni enyi milango ya kale,
ili Mfalme mtukufu aingie.
10Ni nani huyo Mfalme mtukufu?
Ni Mwenyezi-Mungu, wa majeshi,
yeye ndiye Mfalme mtukufu.