Ezekieli 1

Ezekieli 1

Kiti cha enzi cha Mungu

1Mnamo siku ya tano ya mwezi wa nne, mwaka wa thelathini, nilikuwa Babuloni kwenye mto Kebari miongoni mwa wale watu waliopelekwa uhamishoni. Basi, mbingu zilifunguka, nikaona maono ya Mungu.[#1:1 Au “Nilipokuwa na miaka thelathini”. Katika kitabu cha Ezekieli tarehe zinahesabiwa kwa kuzihusisha na wakati mfalme Yehoyakini alipopelekwa uhamishoni (isipokuwa tu 24:1 ambapo yahusu mwaka wa 9 wa utawala wa Sedekia kama ilivyo katika 2Fal 25:1). Kulingana na maelezo zaidi yanayotolewa katika aya ya pili, wakati huo ni mwaka 593 K.K. Baadhi ya wafafanuzi wa Biblia wanafikiri yahusu umri wa nabii wakati wa tukio hilli. Kwa kuliwekea tarehe ni dhahiri kwamba nabii analiona tukio hili kuwa muhimu sana.; #1:1 Au: “mfereji wa Kebari”; yamkini yahusu mojawapo ya mifereji ya mto Eufrate ambao hupitia karibu na mji wa Babuloni.; #1:1 Namna ya kawaida ya kuelezea kutokea kwake Mungu. Kwa matumizi ya mbingu kama makao ya Mungu taz Mwa 28:12; Isa 64:1; Mat 3:16; Mate 7:56; 10:11; Ufu 4:1. “Nikaona maono ya Mungu”: Msemo kawaida wa kutaja ufunuo wa mambo yasiyo ya ulimwengu huu.; #1:1—24:27 Sura hizi (1-24) zahusu kipindi cha kwanza cha huduma ya nabii. Nabii Ezekieli ni “mwonyaji” wa watu wa Mungu (3:26). Nabii anawaonya waachane na maovu yao, wamrudie Mungu wapate angalau kuepa adhabu wanayokabiliwa nayo kwa sababu ya dhambi zao. Sehemu hii inaanza na ono la kuzindua rasmi wadhifa wa nabii (1:1-3:15). Baada ya huo uzinduzi wa nabii vinafuata vitendo ishara kadhaa: Mji wa Yerusalemu utazingirwa hakika (4:1-15). Watu wataangamizwa na wengine watapelekwa uhamishoni. Katika sura ya 6—7 wanaoabudu sanamu za miungu wanalaumiwa na kutangaziwa adhabu. Uhakika wa adhabu hiyo unatiliwa mkazo kwa maono ya sura 5:1-4. Katika sura nyingine zinazosalia (isipokuwa sura ya 18 ambayo inasema juu ya uwezekano wa kuokoka) shutuma dhidi ya maovu ya watu wa Israeli, kadhalika na maovu ya watu wa mataifa mengine zinatolewa na kuelezwa.]

2Katika siku hiyo ya tano ya mwezi (ulikuwa mwaka wa tano baada ya mfalme Yehoyakini kupelekwa uhamishoni Babuloni),

3Mwenyezi-Mungu aliongea nami kuhani Ezekieli mwana wa Buzi, nilipokuwa Kaldayo karibu na mto Kebari, naye Mwenyezi-Mungu akaniwekea mkono wake.[#1:3 Au “nchi ya Wakaldayo”; Kiebrania “Kasdi”. Dola la Wakaldayo, mara nyingine hutajwa kama Babuloni-mpya; ilianzishwa na mfalme mmoja aitwaye Nabopolasa yapata mwaka 626 K.K.; #1:3 Hii ni namna ya kusema anayotumia nabii Ezekieli mara kadhaa kuashiria kwamba alikuwa anaoongozwa kwa nguvu yake Mwenyezi-Mungu mwenyewe. Hapa maneno hayo yanatumika mara ya kwanza aghalabu kuashiria kwamba Mwenyezi Mungu anamchagua Ezekieli kuwa nabii au msemaji wake. Tazama pia matumizi ya msemo huo huo katika mazingira ya maandishi ya 33:22 na 37:1. Rejea pia 3:14,22; 8:1; 40:1.]

4Nilipotazama niliona upepo wa dhoruba unavuma kutoka kaskazini: kulikuwa na wingu kubwa lililozungukwa na mng'ao, na moto ulichomoza humo mfululizo na katikati ya huo moto kulikuwa na kitu kinametameta kama shaba.

5Kutoka humo nilibainisha viumbe hai wanne, ambao walionekana hivi: Walikuwa na umbo la binadamu.

6Kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne.

7Miguu yao ilikuwa imenyoka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa.

8Walikuwa na mikono ya binadamu chini ya mabawa yao katika pande zao nne.

9Ncha za mabawa yao ziligusana kila bawa na bawa lingine. Waliposogea, upande wowote ule, walikwenda mbele moja kwa moja bila kugeuza miili yao.

10Kuhusu nyuso zao nne kila mmoja wao alikuwa na uso wa binadamu upande wa mbele, uso wa simba upande wa kulia, uso wa ng'ombe upande wa kushoto, na uso wa tai upande wa nyuma.

11Mabawa mawili ya kila mmoja yalikuwa yamekunjuliwa juu na kugusana na kwa mabawa yale mengine mawili walifunika miili yao.[#1:11 Labda hivyo; Kiebrania hapa ni kigumu kuelewa.]

12Popote roho ilipotaka kwenda, walikwenda; kila mmoja wao alikwenda mbele moja kwa moja bila kuugeuza mwili wake.[#1:12 Tafsiri nyingine “Popote walikotaka kwenda, walikwenda.”]

13Katikati ya hao viumbe hai kulikuwa na kitu kilichoonekana kama makaa yanayowaka moto, kama miali ya moto iliyomulika huku na huko kati ya hao viumbe. Moto huo ulikuwa mwangavu na umeme ulichomoza humo.[#1:13 Katika Kiebrania aya hii ya 13 ni ngumu sana kuelewa.]

14Viumbe hao pia walikwenda huku na huko kama pigo la umeme.[#1:14 Au “kama cheche zirukazo motoni”.]

15Nilipokuwa nawatazama hao viumbe hai niliona chini karibu na kila kiumbe kulikuwa na gurudumu.[#1:15 Tafsiri kulingana na hati nyingine za kale. Kiebrania “karibu na nyuso zao”.; #1:15 Maana ya Kiebrania cha aya hii ni ngumu.]

16Magurudumu hayo yalionekana kuwa ya namna moja, yanametameta kama jiwe la zabarajadi na muundo wao ulikuwa kama gurudumu ndani ya gurudumu lingine.[#1:16 Kito kama yakuti rangi zambarao-kijani.; #1:16 Au “gurudumu ndogo ndani ya gurudumu lingine”. Kiebrania si dhahiri.]

17Yaliposogea yalikwenda upande wowote wa pande nne za dira ya dunia bila kugeuka.

18Mizingo ya hayo magurudumu ilikuwa mirefu kutisha na mizingo ya magurudumu hayo ilikuwa imejaa macho pande zote.[#1:18]

19Hao viumbe hai walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda kandokando yao; na viumbe hao walipoinuka juu kutoka ardhini, magurudumu hayo yaliinuka.

20Popote roho ilipokwenda walikwenda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao; maana roho ya hao viumbe hai ilikuwa katika magurudumu hayo.

21Viumbe hao walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda; waliposimama, nayo yalisimama; walipoinuka juu kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka pamoja nao. Maana roho ya hao viumbe hai ilikuwa katika magurudumu hayo.

22Juu ya vichwa vya hao viumbe hai kulikuwa na kitu mfano wa anga, kinang'aa kama kioo.[#1:22 Kiebrania “anga linalotisha”.]

23Chini ya kitu hicho walisimama hao viumbe hai; mabawa mawili ya hao viumbe yalikuwa yamekunjuliwa kuelekeana, na kwa mabawa mengine mawili walifunika miili yao.

24Walipokuwa wanakwenda, nilisikia sauti ya mabawa yao; sauti ya mvumo huo ilikuwa kama ile ya maji mengi, kama sauti ya ngurumo kutoka kwa Mungu wa majeshi, na kama kelele ya jeshi kubwa. Waliposimama, walikunja mabawa yao.

25Nilisikia sauti kutoka juu ya kitu kile kama anga kilichokuwa juu ya vichwa vyao.

26Juu ya kitu hicho niliona kitu kama kiti cha enzi cha johari ya rangi ya samawati. Juu yake aliketi mmoja anayefanana na binadamu.[#1:26 Jiwe la thamani rangi samawati au buluu.]

27Sehemu ya juu ya mwili wake iling'aa kama shaba, kama moto uliozunguka pande zote; sehemu ya chini ya mwili wake ilikuwa kama moto nayo ilizungukwa na mng'ao

28ulioonekana kama upinde wakati wa mvua. Ndivyo ulivyoonekana mfano wa utukufu wa Mwenyezi-Mungu. Nilipouona, nilianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania