Hosea 8

Hosea 8

Makosa makuu ya Israeli

1“Pigeni baragumu!

Adui anakuja kama tai

kuivamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu,

kwa kuwa wamelivunja agano langu

na kuiasi sheria yangu.

2Waisraeli hunililia wakisema:

‘Mungu wetu, sisi tunakujua.’

3Lakini Israeli amepuuza mambo mema,[#8:3 Rejea Mika 6:8.]

kwa hiyo, sasa adui watamfuatia.

4“Walijiwekea wafalme bila kibali changu,

walijiteulia viongozi ambao sikuwatambua.

Wamejitengenezea miungu ya fedha na dhahabu,

jambo ambalo litawaangamiza.

5Watu wa Samaria, naichukia sanamu yenu ya ndama.[#8:5 Yahusu ile sanamu ya ndama ambayo Yeroboamu aliisimika kule Betheli (1Fal 12:18-20; Hos 10:5).]

Hasira yangu inawaka dhidi yenu.

Mtaendelea mpaka lini kuwa na hatia?

6Nanyi Waisraeli ni hivyohivyo!

Na sanamu yenu hiyo fundi ndiye aliyeitengeneza.

Yenyewe si Mungu hata kidogo.

Naam! Sanamu ya ndama ya Samaria itavunjwavunjwa!

7“Wanapanda upepo, watavuna kimbunga![#8:7 Maneno yanayofanana na yale ya Yobu 4:8; Meth 22:8; Hos 10:13. Huenda Hosea alimaanisha kwamba mahali pa upepo wangalipaswa kushughulikia haki wapate kuvuna upendo. Upepo hapa waweza kumaanisha udanganyifu. Taz Mhub 1:14,17; Meth 11:29; Yobu 77:1, wanajidanganya kuabudu sanamu.]

Mimea yao ya nafaka iliyo mashambani

haitatoa nafaka yoyote.

Na hata kama ikizaa,

mazao yake yataliwa na wageni.

8Waisraeli wamemezwa;

sasa wamo kati ya mataifa mengine,

kama chombo kisicho na faida yoyote;

9kwa kuwa wamekwenda kuomba msaada Ashuru.

Efraimu ni punda anayetangatanga peke yake;

Efraimu amekodisha wapenzi wake.

10Wametafuta wapenzi kati ya watu wa mataifa,

lakini mimi nitawakusanya mara.

Na hapo watasikia uzito wa mzigo,

ambao mfalme wa wakuu aliwatwika.

11“Watu wa Efraimu wamejijengea madhabahu nyingi,

na madhabahu hizo zimewazidishia dhambi.

12Hata kama ningewaandikia sheria zangu mara nyingi,

wao wangeziona kuwa kitu cha kigeni tu.

13Wanapenda kutoa tambiko,

na kula nyama yake;

lakini mimi Mwenyezi-Mungu sipendezwi hata kidogo.

Mimi nayakumbuka makosa yao;

nitawaadhibu kwa dhambi zao;

nitawarudisha utumwani Misri.

14Waisraeli wamemsahau Muumba wao,[#8:14 Rejea Isa 44:2; 51:13.]

wakajijengea majumba ya fahari;

watu wa Yuda wamejiongezea miji ya ngome,

lakini mimi nitaipelekea moto miji hiyo,

na kuziteketeza ngome zao.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania