The chat will start when you send the first message.
1Yesu aliwaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia.
2Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi.[#14:2 Yesu anaongea hapa juu ya mbinguni. Taz pia Orodha ya Maneno.]
3Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi.
4Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda.”
5Thoma akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?”[#14:5 Mmoja wa wanafunzi 12 (taz Mat 10:3). Anaitwa pia Pacha, neno ambalo ni tafsiri ya Thoma kutokana na Kiaramu. Picha inayotolewa katika Injili ya Yohane ni kwamba huyu Thoma alikuwa mtu wa mashakamashaka (taz pia 20:24-29).]
6Yesu akamjibu, “Mimi ni njia, na ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu.[#14:6 Yesu ni njia ya kwenda kwa Mungu; yeye ni ukweli wote juu ya Mungu na matakwa yake kuhusu binadamu; yeye ni uhai (rejea Yoh 1:4; 3:16; 11:25; 17:3; taz pia Yoh 6:35). Binadamu ataweza kwenda kwa Mungu Baba kwa kupitia kwa Yesu Kristo peke yake (Mat 11:27; Yoh 1:18; 6:46; Mate 4:12).]
7Ikiwa mnanijua mimi, mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona.”
8Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, nasi tutatosheka.”
9Yesu akamwambia, “Nimekaa nanyi muda wote huu, nawe Filipo hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: ‘Tuoneshe Baba?’
10Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake.
11Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya.
12Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, kwani ninakwenda kwa Baba.[#14:12 Yesu anaporudi kwa Baba (7:33; 13:1; 14:28) atawajalia wafuasi wake uwezo wote wa Roho wa Mungu (7:39), ambao utawawezesha kutenda makuu zaidi hata kuliko yeye!]
13Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
14Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.
15“Mkinipenda mtazishika amri zangu.
16Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele.[#14:16 Neno lililotafsiriwa hapa kama Msaidizi ni “parakletos” katika Kigiriki nalo laweza pia kuwa na maana ya “mwombezi” (taz 1Yoh 2:1) au “wakili”. Roho Mtakatifu atachukua nafasi ya Yesu mwenyewe kama kiongozi na mwalimu wa wanafunzi wake (taz pia 14:26; 15:26; 16:7).; #14:16-17 Hapa inasemwa Msaidizi mwingine, yaani Yesu naye pia ni Msaidizi au Mwombezi au Mtetezi (taz 1Yoh 2:1 ambapo Yesu anaitwa moja kwa moja kwa jina hilo la Kigiriki “parakletos” yaani, Mwombezi, Mtetezi au Wakili, Msaidizi).]
17Yeye ni Roho wa ukweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini nyinyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.[#14:17 Taz 12:31 maelezo.]
18“Sitawaacha nyinyi yatima; nitakuja tena kwenu.
19Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini nyinyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai.
20Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu.
21Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
22Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, “Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”[#14:22 Huenda ni sawa na Yuda mwana wa Yakobo anayetajwa katika Luka 6:16; Mate 1:13.]
23Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye.
24Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.
25“Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi,
26lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni.
27“Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.[#14:27 Amani ambayo Yesu anawapa wanafunzi wake ni zaidi ya hali isiyo na misukosuko ya ndani na nje. Amani hiyo ni hali njema kamilifu ya roho na mwili.]
28Mlikwisha sikia nikiwaambieni: ‘Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi.
29Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini.
30Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu;[#14:30 Yaani Shetani (taz 12:31 maelezo; 13:2,26,27; 16:11; Ufu 20:2-3,7-10).]
31lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!