The chat will start when you send the first message.
1Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,[#21:1 Kijiji kimoja upande wa mashariki wa mlima wa Mizeituni kuelekea Bethania (taz 21:17); kwa sasa ni Kefr-et-Tur.; #21:1 Mlima upande wa Mashariki wa mji Yerusalemu, karibu kilomita moja kutoka mjini (Mate 1:12).; #21:1-22 Sehemu hii yaweza kueleweka kama vitendo vitatu vya ishara (mithili ya vitendo vya ishara vya baadhi ya manabii; rejea vitendo vya ishara vya manabii, k.m. Eze 4:1—5:4): Aya 1-11: Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe, akitajwa kama Masiha na mfalme. Aya 12-17 Yesu analitakasa hekalu na hivyo kuonesha kwa ishara hiyo kwamba yeye anayo mamlaka juu ya ibada za Wayahudi. Aya 18-22 Yesu anaulaani mtini, kitendo ambacho labda ni ishara ya laana kwa viongozi wa Waisraeli ambao hawakupokea ujumbe wa Yesu.]
2akawaambia, “Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu.[#21:2 Yaonekana mwandishi aliielewa ile sehemu ya kitabu cha Zekaria (Zek 9:9) kwamba ilihusu wanyama wawili. Injili nyingine zinataja mmyama mmoja tu (Marko 11:3; Luka 19:30; Yoh 12:14).]
3Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji,’ naye atawaachieni mara.”[#21:3 Au, “Mwenyewe anawahitaji”. Neno la Kigiriki mara nyingi hutumika kwa maana ya “Bwana” ambaye hao punda ni wake; lakini si yamkini kwamba Yesu angetumia maneno hayo kwa maana hiyo.]
4Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie:
5“Uambieni mji wa Siyoni:
Tazama, Mfalme wako anakujia!
Ni mpole na amepanda punda,
mwanapunda, mtoto wa punda.”
6Hivyo, wale wanafunzi walikwenda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza.
7Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake.
8Umati mkubwa wa watu wakatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani.[#21:8 Vitendo hivyo vilikuwa vya kumkaribisha. Watu makundi kwa makundi walikuwa wamekuja kutoka Galilaya na sehemu nyingine kwa sikukuu ya Pasaka.]
9Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti:
“Sifa kwa Mwana wa Daudi!
Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana!
Sifa kwa Mungu juu!”
10Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, “Huyu ni nani?”
11Watu katika ule umati wakasema, “Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti mji wa Galilaya.”
12Basi, Yesu akaingia hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa.[#21:12 Ndani ya ukumbi wa nje wa hekalu, sehemu ambayo watu wasio Wayahudi waliweza kuingia, kulikuwa na wafanyabiashara ambao kazi yao muhimu ilikuwa kubadilisha fedha kwa ajili ya kuwapatia watu fedha iliyotakiwa kwa zaka na kuuza wanyama waliohitajika kwa sadaka (Mat 17:14). Shughuli hizo mara nyingi ziliwapa wengine fursa ya udanganyifu (aya 13).]
13Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala.’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.”
14Vipofu na vilema wengine walimwendea huko hekaluni, naye Yesu akawaponya.
15Basi, makuhani wakuu na waalimu wa sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaza sauti zao hekaluni wakisema: “Sifa kwa Mwana wa Daudi,” wakakasirika.
16Hivyo wakamwambia, “Je, husikii wanachosema?” Yesu akawajibu, “Naam, nasikia! Je hamjapata kusoma Maandiko haya?
‘Kwa vinywa vya watoto wadogo na wachanga
wajipatia sifa kamili.’”
17Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko.[#21:17 Kijiji kimoja mashariki ya mlima wa Mizeituni, yapata kilomita 3 kutoka mjini Yerusalemu; kwa sasa ni El-azariye.]
18Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa.
19Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauna chochote ila majani matupu. Basi, akauambia, “Usizae tena matunda milele!” Papo hapo huo mtini ukanyauka.[#21:19 Katika Marko 11:12-14,20-25 mtini huo ulionekana siku ya pili umenyauka.]
20Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, “Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?”
21Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: ‘Ng'oka ukajitose baharini,’ itafanyika hivyo.[#21:21 Kuhusu Mtindo huu wa kusema hapa, ambao karibu ni kama kitendawili, taz Mat 17:20 maelezo na pia rejea 1Kor 13:2.]
22Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba kwa sala, mtapata.”
23Yesu aliingia hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?”[#21:23 Swali hilo limetokana na matendo ya Yesu kama yalivyotajwa katika aya ilyotangulia. Taz 21:1-22 maelezo.]
24Yesu akawajibu, “Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.
25Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?” Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’
26Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu,’ tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii.”
27Basi, wakamjibu, “Hatujui!” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.
28“Nyinyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’
29Yule kijana akamwambia, ‘Sitaki!’ Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi.
30Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, ‘Naam baba!’ Lakini hakuenda kazini.
31Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?” Wakamjibu, “Yule mtoto wa kwanza.”
Basi, Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, watozaushuru na waasherati wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu.
32Maana Yohane alikuja kwenu akawaonesha njia adili ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watozaushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote nyinyi hamkutubu na kumsadiki.”[#21:32 Yohane aliwatangazia watu matakwa ya Mungu. Taz Mat 3:15 maelezo; rejea pia Luka 3:12-14; 7:29-30.; #21:32 Luka 3:12; 7:29-30.]
33Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali.[#21:33 Ilikuwa kawaida kutumia maneno hayo kama mfano wa taifa la Israeli (rejea Isa 5:1-7) ambapo picha hiyohiyo inatumika. Yesu anatumia mfano huo kama kielelezo na wasikilizaji wake wanaelewa mara moja kwamba alikuwa anawasema wao (aya 45).; #21:33 Namna ya kibanda kilichotumika kwa kulinda shamba.]
34Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake.
35Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe.
36Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile.
37Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: ‘Watamjali mwanangu.’
38Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: ‘Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!’
39Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua.[#21:39 Kuuawa kwa huyo mwana wa Mwenye shamba nje ya hilo shamba labda ni wazo linaloendana na kuuawa kwa Yesu nje ya mji wa Yerusalemu. Rejea Ebr 13:11-12 maelezo]
40“Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?”
41Wao wakamjibu, “Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wake.”
42Hapo Yesu akawaambia, “Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu?
‘Jiwe walilokataa waashi
sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.
Bwana ndiye aliyefanya jambo hili,
nalo ni la ajabu sana kwetu!’
43“Kwa hiyo nawaambieni, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake.”[#21:43 Baadhi ya hati za kale zina aya 44: “Mtu yeyote akianguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda”, taz Luka 20:18. Rejea Isa 8:14-15; Dan 2:34-35,44-45.]
45Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia hiyo mifano yake walitambua kwamba alikuwa anawasema wao.
46Kwa hiyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni, lakini waliwaogopa watu kwa sababu wao walimtambua yeye kuwa nabii.