Mathayo 9

Mathayo 9

Yesu anamponya mtu aliyepooza

(Marko 2:1-12; Luka 5:17-26)

1Yesu alipanda mashua, akavuka ziwa na kufika katika mji wake.[#9:1 Au “kijiji chake”. Kadiri ya Marko 2:1 kijiji au mji huo ni Kafarnaumu.]

2Hapo watu walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Jipe moyo mwanangu! Umesamehewa dhambi zako.”[#9:2 Luka 7:48; taz Marko 2:5.]

3Baadhi ya waalimu wa sheria wakaanza kufikiri, “Mtu huyu anamkufuru Mungu!”[#9:3 Kadiri ya Marko 2:7 watu walifikiri hivyo kwa vile Yesu aliwasamehe watu dhambi, uwezo ambao ulikuwa wa Mungu peke yake.]

4Yesu aliyajua mawazo yao, akasema, “Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu?

5Ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, utembee?’

6Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo duniani wa kuwasamehe watu dhambi.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako.”

7Huyo mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akaenda nyumbani kwake.

8Watu wote katika ule umati walipoona hayo, walishangaa na kuogopa; wakamtukuza Mungu aliyewapa binadamu uwezo wa namna hiyo.

Mathayo anaitwa

(Marko 2:13-17; Luka 5:27-32)

9Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda zake, alimwona mtu mmoja aitwaye Mathayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Basi, Yesu akamwambia, “Nifuate.” Naye Mathayo akainuka, akamfuata.[#9:9 Katika Injili ya Luka anatajwa kuwa “Lawi” (5:27), hali katika Marko 2:14 ni Lawi mwana wa Alfayo.]

10Yesu alipokuwa nyumbani ameketi kula chakula, watozaushuru wengi na wahalifu walikuja wakaketi pamoja naye na wanafunzi wake.[#9:10 Makala ya Kigiriki yasema nyumbani kwake Yesu, lakini yaweza kueleweka kwamba ni nyumbani kwa Mathayo (taz 9:1).; #9:10 Kadiri ya tamaduni za kale kule Mashariki ya Kati, kama vile pia miongoni mwa makabila mbalimbali hapa Afrika, kula chakula pamoja kunaonesha pia uhusiano kati ya hao wanaoshiriki chakula hicho pamoja.]

11Mafarisayo walipoona hayo, wakawaambia wanafunzi wake, “Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?”[#9:11 Wote waliohusiana kwa namna yoyote ile na utawala wa Kiroma kama vile watozaushuru, Mafarisayo waliwasema watu wa namna hiyo kuwa wenye dhambi.]

12Yesu aliwasikia, akasema, “Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa.

13Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma, wala si tambiko.’ Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi.”[#9:13 Tazama maelezo ya Luka 15:7.; #9:13 Maneno hayo yamekaririwa kutoka Hosea 6:6 (taz pia Mat 12:7; ling Isa 1:10-17; Amo 5:21-24). Hosea anasisitiza kwamba kuwa na huruma na wema ni kitendo muhimu zaidi kuliko kutolea tambiko hekaluni; rejea pia Mat 5:23-24.]

Suala juu ya kufunga

(Marko 2:18-22; Luka 5:33-39)

14Kisha wanafunzi wa Yohane Mbatizaji walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Sisi na Mafarisayo hufunga mara nyingi; mbona wanafunzi wako hawafungi?”

15Yesu akawajibu, “Je, walioalikwa harusini hutakiwa kuomboleza wakati bwana arusi yupo pamoja nao? La, hasha! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.[#9:15 Tafsiri ya neno kwa neno: “wana wa bwana arusi”.; #9:15 Hapa Yesu anagusia kifo chake.]

16“Watu hawatii kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu. Maana kiraka hicho kitararua hilo vazi kuukuu, na pale palipokuwa pameraruka pataongezeka.

17Wala watu hawaweki divai mpya katika viriba vikuukuu. Wakifanya hivyo, viriba hupasuka na divai ikamwagika, navyo viriba vikaharibika. Ila, watu huweka divai mpya katika viriba vipya, na vyote viwili, viriba na divai, vikahifadhiwa salama.”[#9:17 Viriba vilitengenezwa kwa ngozi ya kondoo; vilitumiwa kuchukulia maji (Mwa 21:14-19); kuhifadhia divai (Yos 9:4,13) na kuwekea maziwa.; #9:17 Maana ya msemo huu ni kwamba mapya na ya kale hayachanganyikani; Habari Njema haiwezi kuchanganywa pamoja na mapokeo ya Kiyahudi.]

Binti wa ofisa na mama mmoja wanaponywa

(Marko 5:21-43; Luka 8:40-56)

18Yesu alipokuwa akisema hayo, ofisa mmoja Myahudi alifika, akamwinamia na kusema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini, tafadhali twende umwekee mkono wako naye ataishi.”[#9:18 Katika Marko 5:22 na Luka 8:41 anatambuliwa kuwa ni Yairo, mkuu wa sunagogi.]

19Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake, akamfuata.

20Mama mmoja, mgonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake.

21Alifanya hivyo kwani alifikiri moyoni: “Nikigusa tu vazi lake, nitapona.”

22Basi, Yesu akageuka akamwona, akamwambia, “Binti, jipe moyo! Imani yako imekuponya.” Mama huyo akapona saa ileile.[#9:22 Au “imekuokoa”.]

23Kisha Yesu akaingia nyumbani kwa yule ofisa. Na alipowaona wapiga filimbi na umati wa watu wanaoomboleza,[#9:23 Kufuatana na tamaduni za huko Palestina wakati huo, hao waliandamana na watu walioagizwa kuomboleza matanga ambayo yalianzia nyumbani kwa mfiwa.]

24akasema, “Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu.” Nao wakamcheka.

25Basi, umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana mkono, naye akasimama.

26Habari hiyo ikavuma sana katika nchi ile yote.

Yesu anawaponya vipofu wawili

27Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda, vipofu wawili walimfuata wakipiga kelele, “Mwana wa Daudi, utuhurumie!”[#9:27 Jina la sifa la yule ambaye ndiye Masiha ambaye Mungu aliahidi kumtuma kwa Wayahudi (Mat 1:1; 15:22; 20:30-31; 21:9,15).]

28Yesu alipoingia nyumbani, watu hao wawili wakamwendea, naye akawauliza, “Je, mnaamini kwamba naweza kuwafanyia jambo hilo?” Nao wakamjibu, “Naam, Bwana.”

29Hapo Yesu akayagusa macho yao, akasema, “Na iwe kwenu kama mnavyoamini.”

30Macho yao yakafunguliwa. Naye Yesu akawaonya kwa ukali: “Msimwambie mtu yeyote jambo hili.”[#9:30 Taz Marko 1:34 maelezo.]

31Lakini wao wakaondoka, wakaeneza habari za Yesu katika nchi ile yote.

Yesu anamponya bubu

32Watu walipokuwa wanakwenda zao, wengine walimletea Yesu mtu mmoja aliyekuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo.

33Mara tu huyo pepo alipotolewa, mtu huyo aliyekuwa bubu akaanza kuongea tena. Watu wakashangaa na kusema, “Jambo kama hili halijapata kuonekana katika Israeli!”

34Lakini Mafarisayo wakawa wanasema, “Anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo wabaya.”[#9:34 Yaani Shetani. Wapinzani wa Yesu walidai kwamba uwezo wa Yesu wa kufukuza pepo wabaya haukutoka kwa Mungu bali kwa Shetani (10:25; 12:24; Marko 3:22; Luka 11:15).]

Yesu anawaonea watu huruma

35Yesu alitembelea miji yote na vijiji, akafundisha katika masunagogi yao akihubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila namna.

36Basi, alipowaona watu, makundi kwa makundi, aliwaonea huruma kwa sababu walikuwa hoi na wenye wasiwasi kama kondoo wasio na mchungaji.

37Hapo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache.

38Basi mwombeni mwenye mavuno atume wafanyakazi wavune mavuno yake.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania