Methali 1

Methali 1

Umuhimu wa methali

1Hizi ni methali za Solomoni mfalme wa Israeli, mwana wa Daudi.[#1:1-7 Huu ni utangulizi wa jumla kwa kitabu chote cha Methali. Mwandishi anatoa lengo la methali nyingi za kitabu hiki, yaani kuwapa watu hekima na nidhamu; kuwafanya waelewe maneno ya busara, kuwa waadilifu na wenye kutenda haki. Juu ya hayo yote, hekima inahusu kumcha Mungu na kutii maagizo yake.; #1:1 Solomoni alisifika kwa hekima yake na anasemekana kuwa alitunga methali nyingi (rejea 1Fal 4:32), ingawa karibu na mwisho wa maisha yake hakuishi kulingana na sifa zake (taz 1Fal 11:1-13). Wafalme waliokuwa na hekima ni wale waliowatawala watu wao kwa haki, uaminifu na sawa (1Fal 3:9-12; Meth 8:12-16; 28:15-16).]

2Methali hizi zawapatia watu hekima na nidhamu; zawafanya waelewe maneno ya busara,

3zawafanya kuwa na nidhamu, utaratibu, uadilifu, haki na kutenda kwa usawa.

4Huwapatia wajinga werevu na vijana maarifa na hadhari.

5Mwenye hekima azisikie na kuongeza elimu yake, naye mwenye busara apate mwongozo.[#1:5 Methali huwafaa sio tu watu wasiokomaa bado na wajinga lakini pia waliokomaa na wenye hekima.]

6Mtu aelewe methali na mifano, maneno ya wenye hekima na vitendawili vyao.[#1:6 Namna moja ya methali iitwayo kitendawili huwa na msingi wake katika suala gumu (Amu 14:12-18) au msemo wenye maana nyingi juu ya hali ya maisha na mafumbo yake (Meth 30:15-16,18-19: 21:23,29-30). Uzoefu wa kutega na kutegua kitendawili ulichukuliwa kuwa ni ishara ya kuwa na busara.]

7Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa maarifa,[#1:7 Kumcha Mwenyezi-Mungu ndio njia ya hekima ya kweli. Katika tamaduni zote za kale kuwa na hekima na busara ilikuwa jambo muhimu sana. Katika kitabu hiki lakini, hekima ina uhusiano na mafundisho ya Mungu. Mtu aliye na hekima ya kweli ni yule anayemcha Mungu na kuishi kadiri ya maagizo yake.]

lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.

Mawaidha kwa vijana

8Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,

wala usiyapuuze mafundisho ya mama yako;

9hayo yatakupamba kilemba kichwani pako,

kama mkufu shingoni mwako.

10Mwanangu, usikubali kushawishiwa na wenye dhambi.[#1:10 Hawa aghalabu ni wale wote wanaokataa kutii mafundisho ya Mungu na mara nyingine katika Methali wanaitwa “wapumbavu” maana dhambi zao huongoza katika kifo (1:32; 9:13-18).]

11Wakisema: “Twende tukamvizie mtu na kumuua;

njoo tukawashambulie wasio na hatia!

12Tutawameza kama Kuzimu wakiwa hai,

watakuwa kama wale washukao Shimoni.

13Tutajitwalia mali zote za thamani,

nyumba zetu tutazijaza nyara.

14Njoo ushirikiane nasi,

vyote tutakavyopata tutagawana.”

15Wewe mwanangu usiandamane nao,

uzuie mguu wako usifuatane nao.

16Maana wao wako mbioni kutenda maovu,

haraka zao zote ni za kumwaga damu.

17Mtego utegwao huku ndege anaona,

mtego huo wategwa bure.

18Wao huvizia na kujiangamiza wao wenyewe,

hutega mtego wa kujinasa wao wenyewe.

19Ndivyo zilivyo njia za waishio kwa ukatili;

ukatili huyaangamiza maisha ya wakatili.

Hekima inaita

20Hekima huita kwa sauti barabarani,

hupaza sauti yake sokoni;

21huita juu ya kuta,

hutangaza penye malango ya mji:

22“Enyi wajinga! Mpaka lini mtapenda kuwa wajinga?

Mpaka lini wenye dharau watafurahia dharau zao,

na wapumbavu kuchukia maarifa?

23Sikilizeni maonyo yangu;

nitawamiminia mawazo yangu,

nitawajulisha maneno yangu.

24Kwa kuwa nimewaita mkakataa kusikiliza,

nimewapungia mkono mje mkakataa,

25mkapuuza mashauri yangu yote,

wala hamkuyajali maonyo yangu,

26nami pia nitayachekelea maafa yenu,

nitawadhihaki mnapokumbwa na hofu,

27hofu itakapowakumba kama tufani,

maafa yenu yatakapowavamia kama kimbunga,

wakati udhia na dhiki vitakapowapata.

28Hapo ndipo mtakaponiita lakini sitaitika;

mtanitafuta kwa bidii lakini hamtanipata.

29Kwa kuwa mliyachukia maarifa,

wala hamkuchagua kumcha Mwenyezi-Mungu;

30maadamu mlikataa shauri langu,

mkayapuuza maonyo yangu yote;

31basi, mtakula matunda ya mienendo yenu,

mtavimbiwa kwa hila zenu wenyewe.

32Maana wajinga hujiua kwa ukaidi wao,

wapumbavu hujiangamiza kwa kujiamini kwao.

33Lakini kila anisikilizaye atakaa salama,

atatulia bila kuogopa mabaya.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania