The chat will start when you send the first message.
1Kwa nini mataifa yanafanya ghasia?[#2:1 Tafsiri nyingine yamkini: “Ya nini … ghasia” Si swali la kujibiwa ila muundo wake ni kwa ajili ya kutilia mkazo kwamba mataifa hayatafanikiwa katika fujo zao.]
Mbona watu wanafanya njama za bure?
2Wafalme wa dunia wanajitayarisha;
watawala wanashauriana pamoja,
dhidi ya Mwenyezi-Mungu na mteule wake.
3Wanasema: “Tujiondoe katika utawala wao;
tutupilie mbali minyororo yao!”
4Mwenyezi-Mungu atawalaye juu mbinguni,
anawacheka na kuwadhihaki.
5Kisha, anawakaripia kwa ghadhabu,
na kuwatisha kwa hasira, akisema:
6“Nimemtawaza mfalme niliyemteua,
anatawala Siyoni, mlima wangu mtakatifu!”
7Mfalme asema: “Nitatangaza azimio la Mwenyezi-Mungu.[#2:7 Kwanza wafalme wanasema (aya ya 3) pili Mwenyezi-Mungu anasema (aya ya 6), kisha hapa, mfalme mteule anasema (aya ya 7).; #2:7 Au, “tangazo” au “mwongozo rasmi” wa Mwenyezi-Mungu. Mfalme alipotawazwa alipewa “sheria” ya Mungu iwe mwongozo wake (taz Kumb 17:18-20; 2Fal 22; 23).]
Mungu aliniambia:
‘Wewe ni mwanangu,
mimi leo nimekuwa baba yako.
8Niombe nami nitakupa mataifa yawe urithi wako,[#2:8 Katika Mashariki ya Kati ya Kale mfalme alipotawazwa, yule aliyemtawaza (mara nyingi akiwa ni kuhani) alitamka mfano huu kwa niaba ya mungu wa mfalme, hali ya kudhihirisha wazi kuwa mfalme ni mwanawe na lazima amtegemee mungu wake. Kwa Waisraeli mfalme ilimpasa amwombe Mwenyezi-Mungu na kumtegemea (Ling 1Fal 3:5 n.k.; 9:1-9; Zab 20:4; 21:2-4).]
na dunia nzima kuwa mali yako.
9Utawaponda kwa fimbo ya chuma;[#2:9 Fimbo ya mfalme (kama vile pia fimbo ya mchungaji wa mifugo) ilikuwa alama ya mamlaka ya kifalme, uongozi na utekelezaji wa haki juu ya watu wake. (Rejea Zab 45:4; 72:1-4; 110:2).]
utawavunja kama chungu cha mfinyanzi!’”
10Sasa enyi wafalme, tumieni busara;
sikilizeni onyo hili, enyi watawala wa dunia.
11Mtumikieni Mwenyezi-Mungu kwa uchaji;[#2:11 Kiebrania ni: “abad” maana yake kidini ni “kuabudu”.]
12msujudieni na kutetemeka;[#2:12 Jinsi tafsiri ilivyo ni kwamba anayesujudiwa ni Mwenyezi-Mungu (12a). Lakini makala ya Kiebrania ni “bar” neno la Kiaramu badala ya neno la Kiebrania “ben” lenye maana ya “mwana”. Hivyo tukitafsiri msujudu mwana (bar), … kutetemeka, yamkini huyo anayesujudiwa hapa ni “ben” na ni rejeleo kwa aya ya 7 ambapo ni “mfalme”, “mwana”, au “Masiha”.]
asije akakasirika, mkaangamia ghafla;
kwani hasira yake huwaka haraka.
Heri yao wote wanaokimbilia usalama kwake!