Zaburi 24

Zaburi 24

Mfalme Mkuu

1Dunia na vyote vilivyomo ni vyake Mwenyezi-Mungu;

ulimwengu na wote waishio humo ni mali yake.

2Maana yeye aliweka misingi ya dunia juu ya bahari;

aliisimika imara juu ya mito ya maji.

3Nani atakayepanda mlima wa Mwenyezi-Mungu?

Nani atakayekaa katika hekalu lake takatifu?

4Ni mtu wa matendo mema na moyo safi,

asiyeuelekeza moyo wake katika upuuzi,

wala kuapa kwa uongo.

5Mtu huyo atapokea baraka kwa Mwenyezi-Mungu,

na haki yake kwa Mungu mwokozi wake.

6Ndio hali ya kizazi cha watu wamtafutao yeye;

naam, watu wamtafutao Mungu wa Yakobo.

7Fungukeni enyi milango;

fungukeni enyi milango ya kale,

ili Mfalme mtukufu aingie.

8Ni nani huyo Mfalme mtukufu?[#24:7-10 Maswali na majibu hapa labda yalikuwa sehemu ya ibada ya zamani watu na makuhani walipoingia hekaluni kwa maandamano.]

Ni Mwenyezi-Mungu, mwenye nguvu na uwezo;

Mwenyezi-Mungu, mwenye uwezo vitani.

9Fungukeni enyi malango,

fungukeni enyi milango ya kale,

ili Mfalme mtukufu aingie.

10Ni nani huyo Mfalme mtukufu?

Ni Mwenyezi-Mungu, wa majeshi,

yeye ndiye Mfalme mtukufu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania