Zaburi 27

Zaburi 27

Kwa Mungu kuna usalama

1Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu,[#27:1 Yaani yeye ndiye anayemwangazia, anayempatia mpango wazi wa maisha na ufahamu.]

ni nani nitakayemwogopa?

Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu,

sitamwogopa mtu yeyote.

2Waovu wakinishambulia,

na kutaka kuniangamiza,

hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka.

3Hata jeshi likinizunguka,

moyo wangu hautaogopa kitu;

hata nikikabiliwa na vita,

bado nitakuwa na tumaini.

4Jambo moja nimemwomba Mwenyezi-Mungu,

nalo ndilo ninalolitafuta:

nikae nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu

siku zote za maisha yangu;

niuone uzuri wake Mwenyezi-Mungu,

na kutafuta maongozi yake hekaluni mwake.

5Siku ya taabu atanificha bandani mwake;

atanificha katika hema lake,

na kunisalimisha juu ya mwamba.

6Nami kwa fahari nitaangalia juu

ya maadui zangu wanaonizunguka.

Nitamtolea tambiko kwa shangwe hekaluni mwake,

nitaimba na kumshangilia Mwenyezi-Mungu.

Msaada wapatikana kwa Mungu

7Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, ninapokulilia,

unionee huruma na kunijibu.

8Moyo wangu waniambia: “Njoo umtafute Mungu!”[#27:8 Kiebrania: “Utafute uso wangu”, yaani kumwendea Mungu katika ibada, kumtegemea na kupata ulinzi wake.]

Basi, naja kwako, ee Mwenyezi-Mungu.

9Usiache kuniangalia kwa wema.

Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako;

wewe umekuwa daima msaada wangu.

Usinitupe wala usiniache, ee Mungu Mwokozi wangu.

10Hata kama wazazi wangu wakinitupa,

Mwenyezi-Mungu atanipokea kwake.

11Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu;

uniongoze katika njia iliyo sawa,

kwa sababu ya maadui zangu.

12Usiniache maadui wanitende wapendavyo;

maana mashahidi wa uongo wananikabili,

nao wanatoa vitisho vya ukatili.

13Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu

katika makao ya walio hai.

14Mtegemee Mwenyezi-Mungu!

Uwe na moyo, usikate tamaa!

Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania