Zaburi 46

Zaburi 46

Mungu yuko upande wetu

1Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu;

yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu.

2Kwa hiyo hatutaogopa chochote,

dunia ijapoyeyuka

na milima kutikisika kutoka baharini;

3hata kama bahari ikichafuka na kutisha,

na milima ikatetemeka kwa machafuko yake.

4Kuna mto ambao maji yake hufurahisha mji wa Mungu,[#46:4-5 Katika Yerusalemu ambao kibiblia ni mji wa Mungu hakuna mto, na wala mto wa pekee kama huu. Maneno hayo yanatumika kimfano. Mto hapa ni ishara au mfano wa uhai. Picha hiyo labda imetolewa kutoka mto wa Bustani ya Edeni (Mwa 2:10). Kuhusu mfano au picha hiyo taz Zab 65:9; Eze 47:1-12; Yoe 3:18; Zek 14:8.]

makao matakatifu ya Mungu Mkuu.

5Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa;

Mungu ataupa msaada alfajiri na mapema.

6Mataifa yaghadhibika na tawala zatikisika;

Mungu anguruma nayo dunia yayeyuka.

7Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi,[#46:7 Mara nyingi jina hili la sifa la Mungu linatumika katika mazingira ambapo sanduku la agano linatajwa na linagusia ukuu na uwezo wa Mungu juu ya maumbile yote.]

Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

8Njoni mwone matendo ya Mwenyezi-Mungu;

oneni maajabu aliyoyafanya duniani.

9Hukomesha vita popote duniani,

huvunjavunja pinde na mikuki,

nazo ngao huziteketeza.

10Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu!

Mimi natukuka katika mataifa yote;

mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”

11Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi,

Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania